NGASSA KUWAKOSA JKT OLJORO KESHO, OKWI MAMBO SAFI


WAKATI mabingwa wa ligi kuu soka  Tanzania Bara, Simba wakishuka katika dimba la Taifa kesho  kuwavaa maafande wa JKT Oljoro, mabingwa hao watamkosa mshambuliaji wao, Mrisho Ngassa.
 Ofisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga aliiambia Sports Lady Blog kwamba Ngassa atashindwa kushuka dimbani kutokana na kusumbuliwa na Malaria. 
Alisema mbali na Ngassa, katika mchezo huo pia watawakosa Haruna Shamte, Haruni Chanongo na Shomari Kapombe ambao wanakabiliwa na majeruhi, huku Amir Maftah ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa jumamosi iliyopita walipokwaana na maafande wa Tanzania Prisons. 
“Ukiacha wachezaji hao, wengine wote waliobaki wako vizuri kabisa na kocha amekiweka sawa kikosi chake kuhakikisha kinashinda mchezo huo na kuzoa pointi tatu muhimu,”alisema Kamwaga. 
Kamwaga aliongeza kuwa, katika mchezo huo  mshambuliaji wao wa kimataifa Emmanuel Okwi ambaye alikuwa akitunimikia adhabu ya kukosa mechi tatu anatarajiwa kuongoza mashambulizi kwa maafande wao hao. 
Alisema mchezo huoutakuwa na ushindani mkubwa kwani Oljoro ni moja ya timu nzuri zinazoshiriki ligi kuu lakini watahakikisha wanaifunga na kujipatia pointi tatu.