Skip to main content

MCHEZO WA MASUMBWI, TAA INAYOZIZIMA – SEHEMU YA SABA


Na Onesmo Ngowi


Masumbwi au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea………………………………….!


            Ni katika miaka ya 40 hadi 70 ambapo mchezo wa ngumi ulivuma sana kwa kutoa mabondia waliosheheni kila aina ya sifa na viwango vizuri vya ngumi. Katika kipindi hiki mashirikisho mengi ya ngumi yalianzishwa na sheria za ngumi pamoja na mifumo yake kubadilika.

Athari nyingi alizokuwa anapata bondia ulingoni zilirekebishwa. Kwa mfano sheria nyingi zililenga kumlinda bondia asidhurike na ngumi alizokuwa anapigwa.

Glovu zilitengenezwa za uzito tofauti na zilizowekwa pamba za kuzuia maumivu makali kwa bondia. Nazo kofia (Head Guards) za kuzuia kichwa kisiumie sana nazo zilianza kutengenezwa na kutumika kwenye mazoezi ambayo mara nyingi ndiyo yanayomuumiza sana bondia kutokana na raundi nyingi anazocheza kwenye sparing!.

Kwa kawaida bondia anatakiwa apigane wastani wa raundi zisizopungua 100 kwa wiki wakati anapojiandaa na mpambano. Mara nyingi anatakiwa apigane na mabondia wenye uzito kuliko yeye ili apate usugu na uzoefu wa kuhimili makonde ya mpinzani wake.

Wapo mabondia wengi waliojizolea sifa kemkem katika kipindi hiki na kuwa mashujaa wa jamii. Kwa kuwa wengi wa mabondia hawa walitoka nchi za Amerika ya Kaskazini na Ulaya waliweza kujulikana sana kwa uwezo wa vyombo vyao vya habari.

Ni kweli kwamba nchi nyingine za Afrika na Asia kulikuwa pia na mabondia wetu waliong’ara katika kipindi hiki kama vile bondia Dick Tiger wa Nigeria ambaye alitokea kuwa tishio kwa mabondia wengine duniani. Bondia huyu alijulikana sana kwa kuwa alihamia Ulaya (Uingereza) na hivyo ilikuwa rahisi kwa vyombo vya habari kumjua na kumtangaza.

Ukosefu wa vyombo vya habari vilivyo na uwezo wa kutangaza dunia nzima uliwakosesha sana mabondia wetu kujulikana ulimwenguni. Japokuwa walikuwa wanajulikana hapa Afrika lakini hawakutajwa kabisa na vyombo vya habari vya nchi zilizoendelea hivyo kuwanyima nafasi kubwa ya kujulikana na mapromota wa mchezo wa ngumi.

Bondia Joe Louis wa Marekani ambaye aliheshimika sana kwa ushupavu wake ulingoni na maisha yaliyopendwa na wengi nje ya ulingo aliongoza kundi hili la mabondia wa wakati wake. Joe Louis aliyekuwa mweusi alipata sana shida kukubalika kwa Wamarekani wote kwani kipindi chake ubaguzi wa rangi ulikuwa umeshamiri sana nchini Marekani.

Pengine ni tabia yake ya kutopenda makuu na ujuzi wake mkubwa ndani ya ulingo yaliyowafanya Wamarekani wa rangi zote wampende kwa kiwango kikubwa.

Akiwa ameweka msingi mzuri uliofuatwa na mabondia wengine kama kina Sonny Liston, Jack Dempsey, Rocky Marciano, Muhammad Ali, Floyd Paterson, Ken Norton, Archie Moore, Jack Quary, Joe Franzier, Joe Burgner, Alexis Anguelo, Leon Spinks,

Wengine ni pamoja na Michael Spinks, George Forman, John Kontey, Alan Minter, Sugar Ray Leonard, Saad Muhammad, Marvin Hugler, Larry Holmes, Tom Heantz, Roberto Duran, Alfred Benitez na wengine wengi.

Mabondia wengi waliotajwa hapo juu walikuwa wa uzito wa juu kwani ni uzito uliokuwa na soko zaidi kwa wakati huo. Mabingwa wengi wa dunia waliolipwa vizuri walikuwa wa uzito wa juu (Heavy).

Katika bara la Afrika mabondia waliowika sana wakati huo japokuwa hawakuwa wa uzito wa juu ni pamoja na Dick Tiger (Nigeria), Philip Waruinge, Dick Tiger Murunga (Kenya) Titus Simba (Tanzania) John Kotey (Ghana) n.k. Miaka ya 80 hadi 2000 Afrika iliweza kuonyesha cheche nyingi katika medani ya kimataifa kwa kutoa mabondia wengi waliojizolea sifa kemkem.

Mabondia hawa japokuwa hawakuwa wa uzito wa juu lakini walivuma sana kwa kutoa upinzani mkali kwa mabondia wengi wa nchi zilizoendelea waliongozwa na Lottie Mwale na Francis Musankabala (Zambia), Steven Muchoki, David Attan, Michael Irungu, Robert Wangila, Isaya Ikonyi, na Modesti Napunyi (Kenya),

Wengine ni Emmanuel Mlundwa, Lucas Msomba, Ahmed Tesha, John Hugo, Clemence Chacha, Isangura, Nassor Michael, Joseph Marwa, Onesmo Ngowi, Gerald Isaac, Ali Muhamed, Emmanuel Kimaro, Rashid Matumla (Tanzania), Ayub Kalule, John Mugabi, John Odhiambo, Boza Edward, John Byaruhanga,  Mustafa Waisaja  na Cuban Businge (Uganda).

Nchi nyingi za kiafrika kama vile DRC, Ethiopia, Afrika ya Kusini, Misri na nyingine nyingi zilikuwa na mabondia wengi waliong’ara sana katika ulimwengu wa masumbwi. Sifa na ushupavu wa mabondia wa wakati ule ni tofauti kabisa na wakati huu.

Miaka ya 70 – 2000 ngumi zilichezwa sana kwa ushindani na uwakilishi wa nchi. Mabondia wengi walipigana kufa na kupona kuwakilisha vyema nchi zao. Ushindi ulipopatikana ulikuwa faraja kwa taifa zima na kila mwananchi alifurahia sana ushindi huo.

Japokuwa hapa Afrika hususan Tanzania mapambano mengi yalikuwa hayaonyeshwi kwenye televisheni, radio nyingi zilitangaza kwa ustadi mkubwa.

Kwa mfano kipindi cha katikati ya miaka ta 70 upinzani mkubwa wa masumbwi katika nchi za Afrika Mashariki ulikuwa kwenye uzito wa Fly, light welter, Welter na middle. Wanamasumbwi waliokuwa wapinzani wakubwa kwa wakati huo ni mabondia Emmanuel Mlundwa, Lucas Msomba, William Lyimo, Ahmed Tesha na Onesmo Ngowi toka Tanzania kwa upande mmoja.

Toka Kenya ni mabondia Stephen Muchoki, George Findo, Modesti napunyi, David Attan na wengine wengi (Kenya). Katika mashindano ya nchi hizi za Afrika Mashariki mabondia hawa na wenzao wa Uganda kama kina John Byaruhanga, John Mugabi, Ayubu Kalule, Cuba Businge, Mustafa Waisaja  na Bonza Edward waliufanya mchezo wa ngumi kuwa na upinzani mkubwa sana.

Mchango mkubwa waliotoa mabondia hawa katika kuuendeleza mchezo wa ngumi unafahamika japokuwa ni tuzo chache sana zilizokwisha tolewa kwao. Lakini sio tabia ya waafrika kuwatuza watoto (wanamichezo) wake. Inafahamika kuwa katika bara al Afrika Nanabii hawaheshimiki kwao!

Nina imani kubwa kuwa mabondia hawa wataingizwa kwenye ECAPBF “Hall of Fame” ikiwa ni juhudi za ECAPBF kuwaenzi wale waliochangia kwenye maendeleo ya ngumi katika ukanda huu. Iaendelea………………………….!

Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail: ibfafrica@yahoo.com