MAAMUZI YA KAMATI YA UCHAGUZI YA TFF


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Oktoba 5, 2012
 
1.           Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika kikao chake kilichofanyika tarehe 03-04 Oktoba 2012 ilijadili michakato ya chaguzi za vyama vya mpira wa miguu vya Mikoa ya Rukwa (RUREFA), Arusha (ARFA), Shinyanga (SHIREFA), Pwani (COREFA), Dar es Salaam (DRFA) na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT). Kamati iliamua yafuatayo:
 
(a)        Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha (ARFA)
Uchaguzi wa ARFA utafanyika  Jumapili, tarehe 07 Oktoba  2012 mjini Arusha kama ulivyopangwa.
 
(b)        Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT)
Uchaguzi wa FRAT utafanyika Jumapili, tarehe 07 Oktoba 2012 mjini Dodoma kama ulivyopangwa.
 
(c)        Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA)
Uchaguzi wa COREFA utafanyika  Jumapili, tarehe 14 Oktoba  2012 Wilayani Mafia kama ulivyopangwa.
 
(d)        Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA)
Kamati ilibaini na kujiridhisha kuwa kulikuwa na udanganyifu uliofanywa na Kamati ya Utendaji ya RUREFA katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba hususan, uteuzi wa baadhi ya  wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA. Pamoja udanganyifu huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imejiridhisha kuwa Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA imeshindwa kutimiza wajibu wake katika kusimamia uchaguzi wa RUREFA, hata baada ya kuwa imepewa onyo kuzingatia matakwa ya Kanuni za Uchaguzi.
 
Kutokana na udanganyifu uliofanyika katika uteuzi wa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa mujibu waKanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 26(2) na (3) na Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), imeamua yafuatayo:
 
(i)  Imeifuta Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA. TFF itateua Kamati mpya ya Uchaguzi ya RUREFA itakayoandaa na kusimamia uchaguzi wa RUREFA.

(ii)Uteuzi wa Kamati mpya ya Uchaguzi ya RUREFA utafanyika wakati muafaka baada ya TFF kukamilisha taratibu za uteuzi, na ratiba ya uchaguzi ya RUREFA itatangazwa baada ya zoezi hilo. 
 
(e)        Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA)
Kamati ya Uchaguzi ya TFF imebaini kuwa baadhi ya viongozi wa Kamati ya Utendaji ya SHIREFA wanaingilia mchakato wa uchaguzi wa SHIREFA kinyume na matakwa ya Kanuni za Uchaguzi  za wanachama wa TFF. TFF haitambui maamuzi ya uongozi wa SHIREFA wa kuivunja Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA inayosimamia uchaguzi wa Chama hicho. Zoezi la uchaguzi wa SHIREFA lililoanza tarehe 08 Septemba 2012 linaendelea na uchaguzi wa viongozi wa SHIREFA utafanyika tarehe 20 Oktoba 2012 kama ulivyopangwa.
 
 (f)         Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es salaam (DRFA)
Kamati ya Uchaguzi ya TFF itakamilisha zoezi la kusikiliza rufaa zilizokatwa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na kupitia mchakato mzima  wa uchaguzi wa DRFA, ili kujiridhisha kama matakwa ya Katiba ya DRFA na TFF yamezingatiwa. Kamati ya Uchaguzi itatoa uamuzi kuhusu rufaa zilizowasilishwa kwenye Kamati kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na kuhusu mchakato wa uchaguzi wa DRFA baada ya kikao chake kitakachofanyika Jumanne, tarehe 09 Oktoba 2012.
 
2.           Kuzingatia Kanuni za Uchaguzi:
 
(i)  Kamati ya Uchaguzi ya TFF itaishauri Mamlaka husika ya TFF kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi wa Kamati za Utendaji walioko madarakani wanaoingilia michakato ya chaguzi za wanachama wa TFF na kusababisha mikanganyiko katika chaguzi ili ama wandelee kuwa madarakani kinyume na matakwa ya Katiba ya TFF Ibara ya 12(2)(a) au wapitishwe kugombea uongozi kinyume na taratibu zilizowekwa na TFF.
 
(ii)Kamati ya Uchaguzi ya TFF inasisitiza na kuzitaka Kamati za Uchaguzi za vyama wanachama wa TFF kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF wakati wote wa michakato ya uchaguzi wa viongozi wa vyama hivyo.
 
 
Angetile Osiah
KATIBU MKUU
KATIBU- KAMATI YA UCHAGUZI –TFF