KIPIGO CHA KAGERA SUGAR CHAIZINDUA YANGA


UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umesema kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar katika mechi ya  juzi, kimewafanya waongeze nguvu ya mazoezi ili kufanya vema katika michezo ijayo.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, licha
ya Yanga kuchezwa kwa juhudi kubwa, ilishindwa kuepuka kichapo cha pili
tangu kuanza kwa ligi hiyo Septemba 15.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, alisema wamepoteza mechi hiyo katika mazingira ya kimchezo.
"Kwa sasa tunajadili nini kilitufanya tushindwe kufanya vizuri katika mechi za mikoani, huku tukiongeza nguvu ya kufanya vema katika mechi zijazo, ukizingatia tuna kocha mpya ambaye ana uwezo mzuri," alisema Mwalusako.
Alisema kitu muhimu kwao ni kujipanga
vizuri zaidi kuelekea mechi ya kesho dhidi
ya Toto Africa ya Mwanza itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.