HASSANOO, KABURU WAPETA COREFA



WANACHAMA maarufu wa klabu ya Simba, Hassan Othman ‘Hassanoo’ na Geofrey Nyange ‘Kaburu’ wamefanikiwa tena kuukwaa uongozi wa chama cha soka mkoa wa Pwani (Corefa). 
Katika uchaguzi huo uliofanyika Wilaya ya Mafia mkoani Pwani jana, Hassanoo alifanikiwa kutetea nafasi yake ya uenyekiti ambaye katika uchaguzi huo hakuwa na mpinzani ambapo alizoa kura zote 22. 
Aidha,Kaburu ambaye ni makamu Mwenyekiti wa Simba, naye aliweza kutetea nafasi yake ya ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kuzoa kura zote 22 za wajumbe walioshiriki kupiga kura. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Corefa, Masau Bwire alisema jana kwamba viongozi hao wapya watakiongoza chama hicho kwa miaka minne, amapo kwa upande nafasi ya Katibu Mkuu ilikwenda kwa Riziki Majala ambaye alipata kura 20 za ndiyo na mbili za hapana. 
Alisema nafasi ya Katibu Msaidizi ilikwenda kwa Mohamed Lubondo aliyepata kura 22, huku Abubakar Allawi aliukwaa Uhazini kwa kura 22, wakati Juma Kisoma alishinda nafasi ya Uwakilishi wa Vilabu (TFF) kwa kura 14 na nafasi ya Mwakilishi kwa upande wa Wanawake ilikwenda kwa Florence Ambonisye aliyezoa kura zote 22. 
Bwire aliwataja wajumbe waliochaguliwa katika kamati ya utendaji ambao wote walizoa kura 22 za ndiyo ni pamoja na Godfrey Haule, Musa Bakari na Gwamaka Mlagila.

Comments