YANGA YAUA 4-0, KWENDA MBEYA J'5


KIKOSI cha timu ya soka ya Yanga kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam jumatano ijayo kwenda mjini Mbeya tayari kwa mechi yao ya fungua dimba ya ligi kuu bara dhidi ya Tanzania Prisons ya huko utakaopigwa katika dimba la Sokoine.
Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesiga Selestine amesema kwamba kikosi cha timu hiyo kipo tayari kwa ajili ya ligi hiyo kwani kupitia mazoezi na michezo ya kujipima nguvu kimeweza kuimarika.
Alisema wachezaji wa timu hiyo ambao wanaendelea na mazoezi yao katika uwanja wa shule ya Sekondari Loyola wapo katika hali nzuri, hali inayowapa matumaini ya kuianza vema ligi hiyo Septemba 15.
“Kikosi chetu kipo vizuri na tayari kwa ligi kuu bara…nadhani jumatano timu itaondoka kwenda Mbeya tayari kwa kuanza ligi kuu”,alisema Mwesiga.
Katika maandalizi yake ya ligi hiyo, Yanga  leo ilicheza mechi ya kujipima ubavu na Moro United katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Mabatini, Kijitonyama jijini Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 ambapo mabao mawili kati ya hayo yalipachikwa na Didier Kavumbagu, huku Shamte Ally na Juma Abdul kila mmoja akifunga bao moja.
Yanga inayonolewa na Mbelgiji Tom Saintfiet pamoja na kucheza mechi kadhaa za kujipima ubavu katika kujiandaa na ligi hiyo ikiwemo ule na African Lyon iliposhinda mabao 4-0,  pia iliiifunga Coastal Union ya Tanga mabao 2-0.
Aidha, Yanga ilifanya ziara ya kimichezo nchini Rwanda na kucheza mechi mbili ambapo ilianza kwa kuifunga Rayon mabao 2-0 kabla ya kuibamiza Polisi ya huko mabao 2-1.