YANGA YACHINJWA, SIMBA YAUA 2-0

YANGA imechapwa mabao 3-0 leo na wenyeji Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Katika mchezo wa leo, Yanga ilizidiwa mno na hadi mapumziko, tayari Mtibwa Sugar walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na beki wa kati, Dickson Daudi dakika ya 11 akiunganisha kwa kichwa kona ya beki wa kushoto Malika Ndeule.
Bao hilo lilitokana na uzembe wa mabeki wa Yanga ambao walishindwa kumuweka ulinzi mchezaji mrefu kuliko wote, Daudi.
Yanga walijaribu kutaka kusawazisha, lakini mipango yao haikuwa na tija na kujikuta wakiendelea kushambuliwa na dakika ya 43, Hussein Javu aliwainua tena vitini mashabiki wa Simba waliokuwa wakiwashangilia kwa nguvu leo kwa kufunga bao la pili.
Kwa ujumla kipindi cha kwanza, Yanga walicheza ovyo- pasi zao nyingi zilikuwa hazifiki, walishindwa kuwabana wapinzani wao na zaidi Haruna Niyonzima alishindwa kuiongoza vema timu, jambo ambalo lilifamnya kiungo mkabaji Athumani Iddi ‘Chuji’ kupanda mbele zaidi kusaidia, ingawa haikusaidia.
Mabeki wawili wa kati wa Mtibwa, Daudi na Salvatory Ntebe waliwadhibiti vema washambuliaji wawili wa Yanga, Hamisi Kiiza na Saidi Bahamnuzi katika dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili, Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet alianza kwa mabadiliko akiwatoa Frank Damayo na David Luhende na kuwaingiza Simon Msuva na Stefano na Mwasyika, lakini bado ukuta wa Mtibwa ulikuwa mgumu mbele ya Watoto wa Jangwani.
Katika kuongeza mashambulizi, Mtakatifu Tom alimtoa beki Mbuyu Twite na kumuingiza na mshambuliaji Didier Kavumbangu, lakini bado mambo yaliendelea kuwa magumu kwa Yanga.
Dakika ya 86 Hussein Javu aliifungia Mtibwa bao la tatu kwa shuti la mbali, wakitoka kushambuliwa na kufikia hapo, Yanga ‘walikufa’ na mashabiki wao wakaanza kuuacha Uwanja wa Jamhuri.
Huu unakuwa mchezo wa pili kwa Yanga tangu kuanza kwa ligi wakiwasononesha mashabiki wao, baada ya mechi ya kwanza kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.   
Waswahili wanasema siku ya kufa nyani, miti yote huteleza, Hamisi Kiiza alipaisha mkwaju wa penalti dakika ya 89, baada ya Daudi kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, , Mbuyu Twite/Kavumbangu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo/Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na David Luhende/Stefano Mwasyika.
Mtibwa Sugar; Shaaban Hassan Kado, Malika Ndeule, Issa R Issa, Dickson Daudi, Salvatory Ntebe, Shaaban Nditi, Jamal Mnyate/Babu Ally Seif, Awadh Juma, Hussein Javu, Shaaban Kisiga ‘Malone’ na Vincent Barnabas/Ally Mohamed ‘Gaucho’.
Katika mechi nyingine,  Simba SC imeendeleza wimbi la ushindi, baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, licha ya kucheza pungufu baada ya Emanuel Okwi kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Mabao ya Simba yalitiwa kimiani na viungo Amri Kiemba na Haruna Moshi ‘Boban’ na kwa matokeo hayo, Simba inaendelea kuongoza ligi kwa kufikisha pointi sita, baada ya awali kuifunga African Lyon 3-0. 
Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Haruna Moshi ‘Boban’, Daniel Akuffo, Mrisho Ngassa na Emanuel Okwi.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Azam imelazimishwa sare ya 2-2 na wenyeji Toto African, Uwanja wa Kaitaba Bukoba, wenyeji Kagera Sugar wametoka sare ya bila kufunga na JKT Oljoro ya Arusha, wakati Uwanja wa Sokoine Mbeya, wenyeji Prisons wametoka sare ya 1-1 na Coastal Union ya Tanga na kwenye Uwanja wa Chamazi, African Lyon imeifunga Polisi Morogoro 1-0, wakati Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Ruvu Shooting imeifunga 2-1 Mgambo JKT. 

Comments