WAKUFUNZI WA WAAMUZI WA FIFA KUANZA KUNOLEWA KESHO


KOZI ya wakufunzi wa waamuzi (Futuro III Refereeing Course) ya Shirikisho la Kimataifa la Soka  (FIFA) inatarajiwa kuanza kesho kwenye hoteli ya Holiday Inn jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura, kozi hiyo itakayoanza saa tatu asubuhi itashirikisha jumla ya washiriki 69 kutoka nchi 21 za Afrika.
Alisema kozi hiyo inayotarajiwa kumalizika Septemba 22 mwaka huu inafanyika katika maeneo mawili ya ufundi (technical) na utimamu wa mwili (fitness).
Alizitaja nchi washiriki ni Afrika Kusini, Botswana, Eritrea, Ethiopia, Gambia, Ghana, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Mauritius, Namibia, Nigeria, Seychelles, Sierra Leone, Somalia, Swaziland, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
“Washiriki kutoka Tanzania kwenye kozi hiyo ni Joan Minja, Leslie Liunda na Soud Abdi (technical) na Riziki Majalla (fitness),”alisema.
Wambura alisema kwamba  baadhi ya wakufunzi wa kozi hiyo wanaotoka FIFA na Shirikisho la soka Afrika (CAF) ni Carlos Henriques anatoka Afrika Kusini, Fernando Gracia (Hispania), Steve Bennett (Uingereza), Tarek Bouchamaoui (Tunisia), James Sekajugo (Uganda), Bester Kalombo (Malawi), Felix Tangawarima (Zimbabwe) na An-Yan Lim Kee Chong (Mauritius).
Aidha, Wambura alisema kozi hiyo itafunguliwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na mjumbe wa Kamati ya Vyama (Associations Committee) ya FIFA.