SIMBA YAANZA NA DOZI, YANGA YATULIZWA SOKOINE

SIMBA SC imeanza vema kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, jioni hii baada ya kuichapa mabao 3-0 African Lyon katika mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyotiwa kimiani na Emanuel Okwi dakika ya 33 baada ya kuwatoka mabeki wa Lyon na Nassor Masoud 'Chollo' dakika ya 36 akiunganisha pasi ya Mrisho Ngassa.
Lyon walikosa penalti dakika ya 35, baada ya mkwaju wa Sunday Bakari kupanguliwa na Juma Kaseja, kufuatia Mwinyi Kazimoto kuunawa mpira kwenye eneo la hatari. 
Kipindi cha pili, Lyon kidogo walirekebisha makosa yao, lakini bado Simba iliendelea kutawala mchezo na dakika ya 56, Danniel Akuffo aliifungia timu yake bao la kuhitimisha ushindi kwa mkwaju wa penalti, baada ya Emmanuel Okwi kuangushwa kwenye eneo la hatari.
Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Haruna Moshi ‘Boban’, Daniel Akuffo/Ramadhan Chombo, Mrisho Ngassa/Abdallah Juma na Emanuel Okwi.
African Lyon; Abdul Seif, Johanes Kajuna, Hamadi Manzi, Sunday Bakari, Benedictor Mwamlangala, Sunday Hinju, Obina Salamusasa, Semmy Kessy, Iddi Mbaga, Jacob Massawe na Yussuf Mlipili.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Yanga imelazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.    
Kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, bao pekee la Abdulhalim Humud liliipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji Kagera Sugar.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, bao pekee la kiungo Mkenya, Jerry Santo dakika ya 41 liliipa Coastal Union ushindi wa 1-0 dhidi ya Mgambo FC.
Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, wenyeji Polisi wamelazimishwa sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar ya Turiani, Manungu.
Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Toto Africans imelazimishwa sare ya 1-1 na JKT Oljoro, wakati Uwanja wa Chamazi, Mbagala, JKT Ruvu imeifunga Ruvu Shooting mabao 2-1.

Comments