SIMBA, TZ PRISONS HAPATOSHI UWANJA WA TAIFA LEO


MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom, Simba leo wanatarajiwa kuwakabili maafande wa Prisons ya Mbeya katika mechi itakayochezwa katika Uwanja
wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Simba, mabingwa watetezi wa ligi hiyo iliyonza Septemba 15, watashuka dimbani wakitaka kuendeleza rekodi ya kutofungwa baada ya kushinda mechi zote tatu, hivyo kuwa na piinti 9.
Hesabu za Simba ni kutaka kushinda mechi ya leo ili kujiweka fiti zaidi kisaikolojia kuikabili Yanga katika mechi ya aina yake itakayopigwa Oktoba 3, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.  
Ofisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema jana kwamba, kikosi cha Simba kipo tayari kwa Mechi ya leo na hakuna kingine wanachokitaraji kutoka kwa Prisons zaidi ya ushindi kabla ya kugeuzia makali hayo kwa Yanga.
Kamwaga alisema kwa vile timu hiyo imepiga kambi Visiwani Zanzibar, itatua jijini Dar es Salaam kwa ndege kisha itarejea huko baada ya mechi hiyo kuzidi kujipanga kwa ajili ya mechi ya Yanga ya hapo Jumatano.
Alisema kupitia kazi kubwa iliyofanywa na Kocha Mkuu, Mserbia Milovan Cirkovic hawana shaka timu hiyo itaendeleza wimbi la ushindi kama walivyofanya kwenye mechi tatu zilizopita tangu kuanza kwa ligi hiyo.
Kuhusu hali ya kikosi, alisema wapo katika hali nzuri isipokuwa Haruna Moshi ‘Boban’ anayesumbuliwa na malaria, hivyo kazi inabaki kwa kocha kupanga nyota wengine watakaoiwezesha kupata pointi zote tatu.
Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa yenye ushindani mkubwa kutokana na kila timu kuwa kuonesha uhai tangu kuanza kwa ligi hiyo, itaanza saa 11 jioni na kurushwa live na kituo cha Televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini.
“Tunafahamu wapinzani wetu  ni moja ya timu bora zinazoshiriki ligi hii lakini kikubwa ni kwamba tumejipanga vema kukabiliana na timu yoyote kwa kuhakikisha tunacheza kwa nguvu zote na hatimaye kushinda,”alisema Kamwaga
Simba inawakabili Prosons wakitoka kuwafunga African Lyon (3-1), JKT Ruvu (2-0)
na Ruvu Shooting mabao 2-1, hivyo leo watakuwa wakipigania ushindi wa nne mfululizo.