SIMBA SC WAREJEA DAR LEO


MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Simba, wanatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam leo kutokea Arusha walikokuwa wamepiga kambi maalumu ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuanza Septemba 15 mwaka huu.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema jana kwamba, mara baada ya kuwasili, wataunganisha kambini moja kwa moja kuendelea na maandalizi yake ya ligi hiyo na keshokutwa watacheza mechi ya kujipima ubavu na Sofapaka ya Kenya.
Alisema, wachezaji wote wapo katika hali nzuri na kupitia kambi ya Arusha, kikosi kimepata maandalizi ya kutosha yakiambatana na mechi kadhaa za kujipima ubavu, hali ambayo inawapa matumaini ya kufanya vema katika michezo yake.
“Tunashukuru kambi imekuwa na mafanikio sana, kwani kikosi chetu kwa sasa ni tishio, hivyo timu zinazoshiriki ligi kuu bara zikae chonjo kwani tutakuja na moto usio na kipimo,” alisema Kamwaga.
Simba itaanza kuvaana na Azam FC katika mchezo wa Ngao ya Jamii  Septemba 11, kabla ya kuanza kampeni zake za kutetea taji lake dhidi ya African Lyon, Septemba 15 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kikosi cha Simba kinachonolewa na Mserbia Milovan Cirkovic, juzi kilikwaana na Soni Sugar ya Kenya na kulazimisha sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.