SIMBA, AZAM FC KUCHANGIA TEMEKE HOSPITALI


Asilimia tano ya mapato yatakayopatikana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kati ya Simba na Azam yatakwenda kwenye Hospitali ya Temeke mkoani Dar es Salaam. 
Kabla ya kukabidhi, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litakutana na uongozi wa Hospitali ya Temeke kupanga maeneo ambayo fedha hizo zitatumika kwenye hospitali hiyo. 
Mechi hiyo ya uzinduzi rasmi wa msimu wa 2012/2013 itafanyika Jumanne ya Septemba 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. 
Viingilio kwenye mchezo huo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa viti vya VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.