SERIKALI YATAKA VAZI LA TAIFA MIAKA 51 YA UHURU


SERIKALI imesema itakuwa vema kama vazi la Taifa likavaliwa rasmi katika maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika itakayoadhimishwa tarehe 9 Desemba, 2012.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara wakati akipokea ripoti ya kamati maalum ya kuratibu upatikanaji wa vazi la Taifa.
“baada ya kuipokea ripoti na kuizingatia kwa makini, mapenda sasa kuelekeza hatua za kuchukua ili mchakato huu wa vazi la Taifa ufikie hatima yake, hata hivyo napenda nichukue fursa hii kuwapongeza kwa dhati wanakamati ya kwa kazi nzuri mliyoifanya hadi kufikia hatua hii ya kutoa ripoti”,alisema
Dk.Fenella ameiagiza Menejimenti ya wizara yake  chini ya usimamizi wa Katibu Mkuu ichague vitambaa vitatu kati ya vitano vilivyopendekezwa na kamati na hivyo vipelekwe ngazi ya sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, kamati ya ufundi ya makatibu wakuu na hatimaye baraza la Mawaziri.
“Pili waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu uteuzi wa kitambaa mwafaka  kwa vazi hilo ufikishwe kwenye baraza la mawaziri ifikapo Oktoba 31, 2012...baada ya hapo viwanda vya nguo nchini vihamasishwe kuzalisha kwa wingi na kwa ubora kitambaa au vitambaa vitakavyokuwa vimeteuliwa ili kushona vazi la Taifa,”alisema
Awali,Katibu wa kamati ya vazi la Taifa Angela Ngowi alisema kamati hiyo ilianza kazi yake mwezi Novemba, 2011 ambapo ilikusanya maoni kutoka kwa wananchi mbalimbali, sambamba na kutumia vyombo vya habari kuhamasisha kuhusina na zoezi hilo.
Alisema katika mchakato wa kupata vazi hilo walipokeza zaidi ya michoro 200 kutoka kwa wasanii 88, kabla ya kamati kupitisha michoro sita ambayo ilikuwa imekidhi vigezo na kuikabidhi kwa wataalamu wa vitambaa na ndipo wakatoa maamuzi yao.
Kamati ya hiyo ipo chini ya mwenyekiti wake Joseph Kusaga, huku Angela Ngowi ni Katibu na Wajumbe ni pamoja na Habibu Gunze, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali, Absalom Kibanda, Makwaia Kuhenga, na Ndesambuka Merinyo.