SERENGETI BOYS YAENDELEA KUJIFUA MBEYA


TIMU ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inaendelea vizuri na kambi ya mazoezi mkoani Mbeya ambapo tayari imecheza mechi moja ya kujipima nguvu.
Kwa mujibu wa Ofisa habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Serengeti Boys jana  ilikwaana  na Tanzania Prisons iliyoko Ligi Kuu ya Vodacom kwenye mji wa Nakonde ulioko mpakani mwa Tanzania na Zambia ambapo timu hizo zilitoka sare ya 1-1 huku bao la Serengeti Boys likifungwa na Miraji Selemani.
Alisema vijana hao leo jioni walitarajiwa kucheza mechi nyingine wilayani Mbozi dhidi ya Mbozi United huku kesho inatarajiwa kucheza mechi yake ya  tatu jijini Mbeya kwa kuikabili  timu ya daraja la kwanza ya Mbeya City.
“Kwa mujibu wa Kocha wa timu hiyo, Jakob Michelsen kambi hiyo inaendelea vizuri, na anatarajia kupata mechi moja ya kirafiki ya kimataifa kabla ya kucheza mechi ya mashindano na Misri, Oktoba 13 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam”,alisema Wambura.