OKWI KUTUA BONGO KESHO

Okwi

MSHAMBULIAJI  wa kimataifa wa Simba Mganda Emmanuel Okwi anatarajia kwasili nchini kesho  kutoka kwao Uganda.
Okwi alikuwa huko kwa ajili ya kuitumikia timu ya Taifa ya huko ‘The Cranes’ ambayo leo ilikuwa na mechi ya kuwania kufuzu fainali za Afrika dhidi ya Zambia.
Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga amesema kwamba wamekubaliana kimaandishi na nyota huyo kwamba atatua leo na kuungana na wenzake wanaojiandaa na ligi kuu bara itakayoanza kutimua vumbi Septemba 15 mwaka huu.
Alisema Okwi pia anatarajiwa kuwepo kwenye kikosi cha Simba kitakachoshuka dimbani keshokutwa kuikabili Azam Fc katika mchezo wa kuwania ngao ya Jamii itakayopigwa katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
 Kamwaga aliongeza kuwa, kikosi cha timu hiyo kipo katika hali nzuri kikiendelea na  maandalizi yake kwa kufanya mazoezi katika viwanja vya TCC Chang’ombe chini ya kocha wake Mserbia Milovan Cirkovic.
Aidha, Kamwaga aliongeza kwamba mshambuliaji wao mwingine wa kimataifa Mzambia Felix Sunzu ambaye alikwenda kwao baada ya kufiwa na dada yake naye alitarajiwa kurejea nchini leo.