MECHI ZA SUPER WEEKEND KUANZA LEO


Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom inaingia raundi ya nne leo  kwa mechi za Super Weekend ambazo zitaoneshwa moja kwa moja (live) na kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini.
 
Mechi ya kwanza ambayo itachezwa leo itakuwa kati ya Azam na JKT Ruvu Stars. Mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itaanza saa 1 kamili usiku kwa viingilio vya sh. 3,000 mzunguko, sh. 5,000 kwa VIP C na VIP B wakati VIP A kiingilio kitakuwa sh. 10,000.
 
Kesho  (Septemba 29 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Simba na Tanzania Prisons itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni. Yanga na African Lyon zitapambana Jumapili (Septemba 30 mwaka huu kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 11 kamili jioni.
 
Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam wenyewe utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar itakayochezwa Oktoba 1 mwaka huu kuanza saa 10.30 jioni. Mechi ya mwisho ya Super Weekend itachezwa Oktoba 3 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikizikutanisha Yanga na Simba kuanzia saa 1 kamili usiku.
 

Comments