Skip to main content

MCHEZO WA MASUMBWI, TAA INAYOZIZIMA – SEHEMU YA TATU‏


Na Onesmo Ngowi


Masumbwi au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea………………………………….!

Mojawapo ya tovuti hizi katika ngumi au michezo mingine zinajulikana kama “Hall of Fame” karibu kila fani / mchezao una “Hall of Fame” yake inayowaonyesha watu mbalimbali waliotoa michango ya kukuza fani husika. Maelezo yanayopatikana kwenye tovuti hizi yanaonyesha kinagaubaga historia na sifa za wanamichezo mbalimbali waliotukuka.

Bondia anayeingizwa kwenye “Hall of Fame” anatakiwa awe ameshatoa mchango wa kutosha kwenye fani ya ngumi na kujizolea sifa kemkem. Lakini sio lazima bondia awe ameshakuwa bingwa tu ndipo aingizwe kwenye “Hall of Fame”. Ipo michezo mingine au fani zilizo na “Hall of Fame” zake mbali na mchezo wa ngumi.


Fani au michezo hii ni pamoja na mpira wa kikapu, riadha, mpira wa miguu, muziki na mpira wa magongo n.k. Kila moja ya fani / michezo hii zina sifa na michango inayotakiwa kwa yeyote anayeingizwa kwenye “Hall of Fame” au kwa maana nyingine“Jumba la Waliotukuka”



Kuingizwa kwenye “Hall of Fame” ya ngumi sio lazima uwe bondia tu bali pia unaweza kuwa mdau wa mchezo wenyewe. Unaweza pia kuwa kiongozi au afisa anayeshughulika kuuchezesha mchezo kama refarii, jaji, mtunza muda, promota, maneja n.k. 




Hii inatokana na ukweli kwamba sio bondia tu anayeendeleza mchezo wa ngumi bali kuna mtiririko wa watu mbalimbali wanaochangia kila mmoja kwa juhudi zake. Ndio maana wadau wote wanaheshimika na michango yao kukumbukwa.




Kwa kuwa mchezo wa ngumi ni mchezo ambao wachezaji hawasaidiwi na mtu mwingine isipokuwa wao wenyewe ndio maana mchezo huu unaheshimika sana. Tofauti na michezo mingine, mchezo wa ngumi ni upinzani kati ya watu wawili tu. 


Ili kuhakikisha kwamba watu hawa hawasaidiwi na yeyote yule wanawekwa kwenye ulingo uliozungushiwa kamba kuzuia watu wengine wasiwaingilie/wasiwasaidie au mmoja wao asitoke nje. 




Aidha washindani wanakuwa na uzito sawa ili kusije kukatokea malalamiko mmoja wao akasema alizidiwa uzito ndio maana akashindwa. Baada ya yote haya wapiganaji huingizwa kwenye ulingo na kutakiwa kupigana. Hii ndiyo tofauti kubwa iliyopo kati ya ngumi na michezo mingine kama mpira wa miguu, mpira wa mikono na michezo mingine mingi.


Kiwango cha upenzi wa mchezo huu hakiwezi kuelezeka lakini siku ambayo pambano kubwa linafanyika kuwakutanisha mabondia wanaojulikana na kuonyeshwa kwenye mitandao ya televisheni inashangaza jinsi idadi kubwa ya watu wanavyoamka usiku wa manane kuungalia. 




Idadi hii inajumuisha pia viongozi mbalimbali katika jamii. Karibu kila mtu mwenye televisheni huamka usiku wa manane na kuutizama mchezo huu. Kila mmoja akitabiri ushindi kwa bondia anayempenda.




Ukitaka kujua watu wanavyoupenda mchezo wa ngumi angalia jinsi watu wanavyochoka asubuhi na mapema makazini kwa kukosa usingizi wakiangalia mpambano wa ngumi. Sio rahisi kuelezea kiwango cha hisia za watu wote wanavyopenda kuangalia mchezo wa ngumi!



MABADILIKO YA MCHEZO WA NGUMI TANGU UANZE KUJULIKANA




Mchezo wa ngumi umekuwa unabadilika jinsi miaka ilivyokuwa inaenda tangu ujulikane. Karne kadhaa kabla ya Kristo ni Warumi walioanza kubadilisha namna mchezo huu ulivyokuwa unachezwa. Kabla ya hapo wachezaji wa mchezo huu walikuwa wanacheza kwa kutumia mikono mitupu na baadaye walifunga vipande vya vyuma katika ngumi zao ili kuzipa makali wanapopigana.




Kwa kawaida matumizi ya kitu chochote kinachoweza kumuumiza mtu yana madhara makubwa sana kwenye mchezo wa ngumi kutokana na sehemu za kichwa panapotakiwa kupigwa. 




Wakati huo ngumi zilichezwa kwa raundi nyingi na mchezo ulikuwa haumaliziki mpaka mmoja wa mpiganaji ashindwe kuendelea au afe. Hii iliwasisimua sana watazamaji na walipiga makelele na kushangilia kwa nguvu zote. 




Wakati Wayunani wanaingiza ngumi kwenye michezo ya mwanzo ya Olimpiki mwaka 776 kabla ya Kristo, sheria mbalimbali zilikuwa zimeshatungwa kuuendesha mchezo huu. Wakati huo katika ulingo kuliongezeka refarii ambaye alihakikisha kuwa wapiganaji wanacheza bila kushikana. Japokuwa wapiganaji walitakiwa wapigane hadi mmoja wao ashindwe kuendelea kabisa lakini ulikuwa mwanzo wa sheria mbalimbali kutumika.




Mabadiliko makubwa ya sheria za ngumi yalianza kutokea katika karne ya 12 wakati sheria za kuuendeleza mchezo huu zilipobadilika kabisa. Kwa kuanzia tu raundi za mchezo wa ngumi zilianza kupungua kutoka kucheza siku nzima na kurudia kesho yake mpaka mmoja wa wapinzani ashindwe kabisa kuendelea na kuanza kuwa raundi 40. Jinsi miaka ilivyokuwa inakwenda sheria hizi nazo zilibadilika na idadi ya raundi nayo ilipungua toka 40 hadi 30 na 20.




Wakati bondia Jack Jonson bingwa wa kutumia mikono mitupu (Bare-Nuckles) wa Marekani alipokuwa bingwa raundi za ngumi zilikuwa ni 20. Huu ndio ulikuwa wakati haswa sheria za ngumi zilipoanza kupata ushirikiano wa kutosha. Iaendelea………………………….!





Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail:ibfafrica@yahoo.com   


Comments