Skip to main content

MCHEZO WA MASUMBWI, TAA INAYOZIZIMA – SEHEMU YA NNE


Na Onesmo Ngowi


Masumbiwi au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea………………………………….! 

 

MATUMIZI YA SHERIA MPYA ZA NGUMI 

                Ni katika mwaka 1866 wakati ambapo mtawala wa Queensbury (Marguees of Queensbury) huko Uingereza alisaidia kutunga sheria mpya zilizotumika kuuendesha mchezo wa ngumi sheria ambazo kwa heshima zilipewa jina lake. Sheria hizi ziliweka bayana mambo yafuatayo:

Uzito wa kila bondia ulianzia Fly ambao ni chini ya kilo 50, bantam kilo 54, featherweight kilo 57, lightweight kilo 60, welterweight kilo 67, middleweight kilo 75, light heavy kilo 80 na hevyweight uzito ambao haukuwa na kikomo.
Sheria za ulingoni: zilipunguza muda uliotumika kwenye raundi za mpambano wa ngumi kuwa dakika 3, na pia ziliweka kikomo kwa mabondia kuangushana chini kama wacheza mieleka. Zilifanya pia matumizi ya gloves kuwa ya lazima. Uzito wa glovu nao ulianzia oz 8, 9, 10, 12 na 15.
Pamoja na ukweli kwamba sheria hizi mpya za hazikuweza kuzuia kwa mara moja kupigana kwa kutumia mikono mitupu (bare-knuckle). Ushindi wa bondia maarufu wa Kingereza James J. Corbet dhidi ya bingwa maarufu aliyejulikana kwa kucheza kwa mikono mitupu John L. Sullivan mwaka 1892 ndipo matumizi ya gloves yalipoanza kutumika rasmi katika mapambano yote ya ngumi.

                Katikati ya karne ya 20 kuelekea kwenye karne ya 21 sheria mpya za ngumi zilitungwa baada ya kuanzishwa kwa mashirikisho mbalimbali ya ngumi ambayo kila moja lilikuja na sheria zake. Kwa uchache sheria hizi zilipunguza raundi za ngumi mpaka kufikia 15 kwa ubingwa wa ngumi na kuweka sheria kali za sehemu ambazo bondia anaweza kumpiga mwingine.

                Aidha sheria hizi ziliweka kikomo katika uzito mbalimbali ambapo kulianzishwa uzito kama light fly, fly, super fly, light welter, junior middle, super middle n.k. Vile vile sheria hizi mpya zilizuia matumizi ya madawa mbalimbali ya kuongeza nguvu kwa mabondia.

Katika mashindano makubwa ya kimataifa hususan Olimpiki wakati wa ngumi za ridhaa sheria za matumizi ya madawa ya kuongeza ngumi ziliwekewa kipaumbele. (Wakati huu madawa mengi ya kuongeza nguvu yamepigwa marufuku karibu katika michezo yote).

                Aidha mabondia mbalimbali ambao waligombea mikanda ya ubingwa walitakiwa walingame uzito na aliyezidi ilibidi apewe muda maalum wa kuupungunza hadi afikie uzito wa mwenzie.

                Ni mwishoni mwa karne ya 20 ndipo mashindano makubwa ya utitiri wa mashirikisho ya ngumi hususan ngumi za kulipwa yalipoanzishwa kwa fujo za aina yake.

Mwanzoni kulikuwepo na shirikisho moja tu nalo lilikuwa Chama cha Ngumi duniani (WBA). Baada ya muda wa miongo kadhaa Baraza la Ngumi Duniani (WBC) nalo lilianzishwa. Mwanzoni mwa miaka ya 80 Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (IBF) nalo lilianzishwa.

                Sababu kubwa ambazo zinatajwa na watu mbalimbali za kuwepo kwa utitiri wa mashirikisho haya ni ubinafsi. Lakini ukiangalia kwa makini kuanzishwa kwa mashirikisho haya kumeweza kwa kiasi kikubwa kuwapa nafasi mabondia wengi kujulikana kimataifa.

Hebu fikiria kuwa katika nafasi ya ubingwa wa shirikiso moja kuna nafasi 17 tu za ubingwa. Kwa maana nyingine mabondia 17 tu ndio wanatakiwa wajulikane kuwa ni mabingwa wa dunia kwa wakati mmoja.

                Idadi kamili ya mabondia walioko dunia nzima haijulikani lakini inaweza kufikia malaki kama sio mamilioni kadhaa. Itakuwa vigumu sana kwa mabondia wote kuweza kufikia ubingwa wa dunia katika maisha yao kama kungekuwepo na shirikisho moja tu.

Japokuwa kuna hisia kuwa mashirikisho mengine yamezidiwa umaarufu na mengine lakini kunasaidia kuwapa nafasi nzuri mabondia wengi kujulikana duniani. Kwa sasa inakadiriwa kuweko kwa mashirikisho kama 15 na ukizidisha kwa 17 utaona tayari mabondia wengi zaidi wanaweza kuwa mabingwa wa dunia kwa wakati mmoja. Japokuwa bingwa mmoja wa dunia anaweza kujulikana kwa zaidi ya shirikisho moja.


SHERIA ZA BAADHI YA MASHIRIKISHO YA NGUMI


Mashirikisho mengi ya ngumi yanatumia sheria zinazofanana. Yote yanatumia sheria za “Marguees of Qunensbury” yaani mabondia wapigane wakiwa wamevaa glovu mikononi zenye uzito unaofanana. Wawe na uzito sawa na ngumi zipigwe kuanzia juu ya mkanda.

Ikumbukwe kuwa mengi ya mashirikisho haya yalianzishwa miaka ya karibuni. Kabla ya shirikisho hata moja la ngumi kuanzishwa ngumi zilikuwa zinatawaliwa (zinaendeshwa) na kamisheni za mitaa, manispaa na nchi mbalimbali. Hata wakati mabondia wa zamani wanatwa ubingwa wa dunia kwao hakukuwa na njia mbadala ya kuwakutanisha na mabondia wengi waliokuwa kwenye viwango vimoja na wanotoka katika nchi mbalimbali.

Ikumbukwe pia kwamba neno ubingwa wa ngumi linamaanisha ushindi wa tuzo katika kiwango chako. Kama unawashinda mabondia karibu wote walio kwenye kiwango chako unakuwa bingwa wa kiwango hicho. Viwango huwekwa na mashirkisho yanayosimamia ngumi.
Kwa mfano mabondia wanaowekwa kwenye viwango fulani vya ngumi wanatakiwa wawe wamecheza mapambano kadhaa yenye hadhi ya kitaifa na kimataifa.

Shirikisho la Ngumu la Kimataifa (IBF) linataka walio kwenye viwangio vyake wawe wameshindana na mabondia wenye hadhi ya kimataifa. Viwango vya IBF vinaanzia 1-15 kila uzito.  Bondia anayeingizwa kwenye viwango vya IBF ni lazima awe amecheza mapambano zaidi ya 15 yenye hadhi ya kimataifa ya kushinda asilimia 75 ya mapambano yote.

Yapo mashirikisho mengine yenye utaratibu tofauti na wa IBF na ambayo masharti ya kuingizwa kwenye viwango vyake sio magumu sana. Pengine ndio maana mashirikisho ya IBF, WBA, WBC na WBO yanaheshimika zaidia duniani kwa kuwa masharti ya kuwekwa kwenye viwango vyake na kucheza ubingwa wake ni magumu zaidi.

Kwa ajili ya sheria kuwa ngumu mashirikisho haya yana makubaliano ya kuwaruhusu mabondia kucheza ubingwa unaotambuliwa na mashirikisho yote manne kwa pamoja (unification titles). Yaani bondia anaweza kugombania ubingwa mmoja unaotambuliwa na IBF, WBA, WBU na WBO na kuvaa mikanda minne. Mabingwa hawa wanajulikana kama undisputed champions (mabingwa wasiopingika)

Sina maana kwamba ubingwa wa mashirikisho mengine hauna maana bali yamezidiana kwa umaarufu na heshina tu. Bingwa wa dunia ni bingwa kwa wapenzi wake na wapinzani wake.

Wako mabingwa wa mashirikisho mengine kama IBA, IBC, WBF, WPBF ambao wamekuja baadaye kuwa mabingwa wa sasa wa WBC, WBA, IBF na WBO. Mfano mmoja ni bingwa wa sasa wa WBC Vitali Klitschko toka Ukraine ambaye kwa muda mrefu alikuwa bingwa wa dunia wa WBO. Iaendelea………………………….!

Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail: ibfafrica@yahoo.com

Comments