KUTEKWA KWA KELVIN YONDAN


KLABU ya soka ya Simba inadaiwa kumteka kwa nguvu beki wa Yanga, Kelvin Yondan.
Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam zinaeleza kwamba zoezi hilo lilifanyika juzi usiku ambapo mchezaji wa zamani wa Simba (jina kapuni) aliendesha zoezi hilo kwa lengo la kumlazimisha kurejea Simba.
Inadaiwa mchezaji huyo wa zamani wa alikwenda nyumbani kwa Yondan na wakati anaondoka aliomba kuendesha gari ya Yondan aina ya Mitsubishi Pajero lakini cha kushangaza mkongwe huyo aliendesha gari na mpaka kwenye ofisi za kiongozi mmoja wa Simba.
“Walipofika huko aliwekewa mil.20 mezani na kutakiwa asaini fomu za kielektronik (Transfer Match System) na ndipo alipotafuta upenyo wa kutoka na kumpigia simu mmoja ya wajumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga Seif Ahmed ili kuomba na msaada,”alisema mtoa habari huyo.
Taarifa zinaongeza kwamba, Yondan alipata upenyo wa kutoka baada ya mwenyeji wao kutoka na kwenda kuwasha gari lake lakini askari walimzuia kabla ya kudanganya kuwa ametumwa vocha na kiongozi huyo wa Simba na ndipo aliporuhusiwa na kuondoka.
Baada ya kuchomoka mikoni mwa watu wa Simba, Yondan alikutana na baadhi ya viongozi wa Yanga na kwenda kituo cha polisi Kilwa na ndipo walipofungua jalada namba KLR/RB/4774/2012.
Gazeti hili lilimtafuta kiongozi wa Simba anayehusishwa kwenye sakata hilo ambapo simu yake iliita bila kupokea kabla ya baadaye kuamua kuizima kabisa.
Hata hivyo, Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema taarifa hizo ni uzushi mtupu kwani zilikuwa na lengo la kuivuruga kamati ya Sheria, Maadili nah ADHI za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa maamuzi yake kuhusiana na suala la mchezaji huyo ambaye Simba ilimuwekea pingamizi.
Kwa upande wa Yanga kupitia kwa katibu wake, Mwesigwa Selestine alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa vile tayari limeshafikishwa katika vyombo vya dola hivyo wanaviachia vifanye kazi yake.
Alipotafutwa kamanda wa polisi wa mkoa wa Temeke David Missime alishangazwa na taarifa hizo na kusema ni uzushi usiokuwa na mashiko ambao alidai ni wa kutafuta umaarufu.
Alisema haiwezekani kumsemea mtu mwenye akili na ingekuwa na mashiko kama mhusika alitekwa na ameshindwa kupatikana au alipatikana akiwa hajitambui ndipo wangeweza kufungua jalada lakini si kwa taarifa za uzushi.

Comments