HASSANOO, AVEVA WAUTAKA UENYEKITI WA SOKA PWANI, DAR


                                                                              Hassanoo
Aveva kulia akiwa na mwenyekiti wa Taswa, Juma Pinto

WANACHAMA maarufu wa klabu ya soka ya Simba, Evance Aveva na Hassan Othaman ‘Hassanoo’ wamejitosa kuwania Uenyekiti wa vyama vya soka vya mikoa ya Dar es Salaam (DRFA) na Pwani (COREFA).
Wakati Aveva akirejesha fomu ya kuwania uenyekiti wa DRFA, Hassanoo amechukua fomu ya kutetea nafasi yake ya Uenyekiti Corefa, katika uchaguzi utakaofanyika mwezi ujao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Aveva ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Simba, alisema ameamua kuwania nafasi hiyo ili kutimiza wajibu wake kama mwana michezo mwenye sifa zinazostahili kuongoza chama chochote cha michezo.
Aveva aliongeza kuwa sababu ya kugombea kwake uongozi ni kutaka kuleta mabadiliko katika chama hicho ambapo kwa kushirikiana na viongozi wenzake iwapo atachaguliwa kukiongoza ana imani kutapatikana mafanikio makubwa.
“Kila mtu ananifahamu mimi kuwa ni mmoja ya wanamichezo wa muda mrefu, pia utendaji wangu wa kazi…nadhani nitaweka wazi mikakati yangu muda wa kampeni utakapofika,”alisema Aveva.
Naye Hassanoo alisema amelazimika kutaka kutetea tena nafasi yake hiyo ili kuendeleza mikakati waliyoianzisha ambapo kwa asilimia kubwa uongozi wake umetimiza uliyoahidi hivyo ni nafasi nyingine tena ya kuufanyia mambo makubwa mkoa wa Pwani.