FOMU COREFA KUANZA KUTOLEWA KESHO


Hassanoo, Mwenyekiti wa Corefa anayemaliza muda wake
WAKATi uchaguzi wa viongozi wa Chama cha soka mkoa wa Pwani (COREFA) ukitarajiwa kufanyika Oktoba 3 Wilayani Mafia, fomu kwa wanaohitaji kuwania nafasi mbalimbali zitaanza kutolewa kesho. 
Akizungumza kwa simu jana, Mwenyekiti wa kamati ya Uchaguzi ya Corefa, Masau Bwire alisema kwamba  fomu hizo zitatolewa kwenye ofisi za chama hicho zilizopo Mailimoja, Kibaha mkoani Pwani na zoezi hilo litafikia tamati Septemba 9 saa kumi jioni. 
Alisema Septemba 10 hadi 15 kamati itapitia fomu za waombaji na kuyabandika kwenye ubao wa matangazo, kabla ya Septemba 16 hadi 20 itakuwa ni wa kupokea pingamizi na Septemba 21 na 22 kamati itajadili pingamizi zitakazo kuwepo.
 Bwire aliongeza kwamba Septemba 23 hadi 25 watatangaza matokeo ya usaili ambapo kwa sasa Hassan Othman Hassanoo ndiye mwenyekiti wa Corefa. 
Alizitaja nafasi zitakazogombewa ni pamoja na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina, Mweka Hazina Msaidizi, Mjumbe Mkutano Mkuu wa TFF, Mwakilishi wa Vilabu TFF, Mjumbe Mwanamke Kamati ya Utendaji na wajumbe watatu wa kamati ya utendaji.