YANGA WAITAKA SIMBA NA RB YA TWITE LEO


WAKATI wingu zito likitanda juu ya kuja nchini kwa beki Mbuyu Twite, uongozi wa Yanga umeibuka na kudai atawasili nchini leo na kuwataka mahasimu wao, Simba, wamsubiri na ‘RB’ wanayodai kuikata ili kumkamata.
Beki huyo, ambaye usajili wake ulizua utata baada ya awali kusaini Simba kwa dola 30,000 za Marekani akipitia timu ya APR ya Rwanda inakodaiwa kuwa alikuwa akicheza kwa mkopo, kabla ya Yanga kuzunguka upande wa pili katika klabu yake ya awali, FC Lupopo ya DRC na kumsainisha kwa dola 50,000.
Kutokana na kusaini Yanga, Twite alituma wawakilishi warejeshe fedha za Simba jijini Dar es Salaam, lakini viongozi wa klabu hiyo waligoma na kumtaka azirejeshe mwenyewe, huku pia wakidai kuwa wamemfungulia jalada polisi na wana ‘RB’ mkononi kwa madai kuwa, mchezaji huyo amefanya kitendo cha wizi wa kuaminiwa.
Kitendo cha Twite kushindwa kutua nchini Jumatatu, Agosti 26 na kikosi cha Yanga alichoungana nacho huko Rwanda kilipokuwa ziarani, kuliibua maneno kuwa beki huyo anagwaya ‘mkwara’ wa Simba.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesigwa Celestine, alisema, Twite atatua Uwanja wa Kimataifa wa JK Nyerere leo na ndege ya Rwanda Air, majira ya saa 9:30 alasiri na kuwataka Simba wamsubiri na RB yao uwanjani hapo.
Akihojiwa hivi karibuni na kipindi cha Spoti Leo cha Radio One, baada ya Yanga kurejea ikitoka Kigali, Rwanda bila Twite, Ofisa Utawala wa Simba, Evodias Mtawala, alisema kuwa, bado wanamsaka nyota huyo, akidai maelezo ya utapeli aliofanya waliyaripoti Polisi Makao Makuu.
Lakini alipoulizwa Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, alishangazwa na madai hayo, kwa maelezo kuwa, Makao Makuu ya Jeshi hayahusiki na utoaji wa RB, na kwamba viongozi Simba wanapaswa kuulizwa walikopata kibali hicho.
“Napenda nikuhakikishie ndugu yangu Makao Makuu ya Polisi hayahusiki na kitu kama hicho. Watafute Simba wakuambie wapi walikofikisha malalamiko yao na kupewa RB,” alisema huku akiongeza kuwa wanaweza kufungua na kupata RB kutoka vituo vya polisi na sio makao makuu.

Comments