WAPYA WA SIMBA KUIVAA MATHARE UNITED KESHO


WACHEZAJI wa kimataifa waliosajaliwa na mabingwa ligi kuu bara Simba, Daniel Akuffo wa Ghana, Komalmbil Keita wa Mali na Mkenya Pascal Ochieng kesho wanatarajiwa kuwemo katika kikosi cha timu hiyo kitachoshuka katika uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kuivaa Mathare United ya Kenya. 
Nyota hao, pamoja na Mganda Mussa Mude, Mzambia Felix Sunzu na Mkenya Emmanuel Okwi ambao Simba imewasajili kwa ajili ya kuichezea katika msimu ujao wa ligi hiyo unaotarajiwa kuanza Septemba 15 na michuano ya kimataifa. 
Hata hivyo uongozi wa Simba , mpaka sasa uongozi haujaweka wazi ni  mchezaji gani kati ya hao atapunguzwa kwani kanuni za ligi kuu zinahitaji timu kusajili wachezaji watano tu wa kigeni ambapo Simba mpaka sasa imesajili nyota sita. 
Shirikisho la soka Tanzania (TFF) juzi lilitangza kupokea hati za uhamisho wa kimataifa (ITC) kwa timu za Ligi Kuu ambapo kwa upande wa Simba imepokea za Mudde na Akuffo, hali inayotia shaka usajili wa Keita na Ochieng kwani Sunzu na Okwi walikuwemo kikosini msimu uliopita. 
Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema kwamba nyota hao watashuka dimbani katika mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa ambapo ni mara yao ya kwanza kucheza tangu wajiunge nayo wiki chache zilizopita. 
Alisema kwamba kikosi cha Mathare kiliwasili tangu jana mjini humo tayari kwa mchezo huo ambao ni maalum kwa kuipa makali Simba ambayo imepiuga kambi mjini Arusha kwa wiki kadhaa sasa kwa ajili ya kujiandaa na ligi kuu bara. 
Alisema, mechi hiyo itamsaidia kocha mkuu wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic kuona mapungufu yaliyopo katika kikosi hicho na kukifanyia marekebisho kabla ya kuivaa Azam Fc Septemba 8 katika mchezo wa kuwania ngao ya Jamii ambao utapigwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 
“Ni kwamba kocha ameomba mechi mbili kabla ya mchezo wetu wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam Fc ili kuweza kufahamu kiwqango cha wachezaji wake…hivyo baada ya mechi hiyo tutamtafutia mchezo mwingine wa kirafiki”, alisema Kamwaga 
Kamwaga aliongeza kuwa, wachezaji wa timu hiyo wapo katika hali nzuri isipokuwa Shomari Kapombe ambaye anaendelea na matibabu, huku msham,buliaji wao wa kimataifa Mzambia Felix Sunzu aliyekuwa akiugua Malaria hali yake ikitengemaa na ameshaanza mazoezi. 
Alisema viingilio katika mchezo utakaoanza saa kumi jioni ni sh 10,000 kwa watakaokaa jukwa kuu, sh 5,000 kwa viti vya kawaida na sh 3,000 katika mzunguko.