WACHEZAJI WANAOTUMIA DAWA ZA KULEVYA KUKIONA CHA MOTO



SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema litaanza kufanyia kazi kwa vitendo tatizo la utumiaji wa dawa za kulevya hususan bangi unaodaiwa kufanywa na baadhi ya wachezaji hapa nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga, alisema miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili ni kile kinachodaiwa kuwa baadhi ya wachezaji wanatumia bangi, ingawa bado hawajapata ushahidi.
“Tunasikia, lakini hatuna ushahidi, kwamba vijana wetu wanatafuna bangi, ila viongozi wengi wamekuwa wakilisemea pembeni, sisi kama wazazi jukumu letu ni kuwaelimisha juu ya athari zake, maana wao wanaotumia wanaweza kuona inawaongezea hamasa, lakini hawajui madhara yake,” alisema Tenga.
Alisema wameagiza suala hilo lianze kufanyiwa kazi katika timu ya taifa, Taifa Stars na Ligi Kuu Bara, ambako viongozi wanapaswa kukaa chini na vijana wao kuwapa elimu nasaha, kabla ya kuanza kuchukuliwa hatua.
“Bangi na mpira ni vitu viwili tofauti, tumeagiza elimu ianze kutolewa kuanzia national team (timu ya taifa) na Premier League (Ligi Kuu), ikiwezekana waletewe hata wataalamu waweze kuwapa elimu kabla hatujaanza kuchukua hatua, ambapo kutakuwa na testing (vipimo) ya kushtukiza na atakayekataa, kanuni zinachukua mkondo wake mara moja,” alisisitiza Tenga.
Tenga aliongeza kuwa, suala hilo litawekwa katika kanuni za Ligi Kuu na tayari Kamati ya Tiba imepewa maelekezo kuhusiana na hilo, ambapo litaanza kufanyiwa kazi mara tu elimu itakapokuwa imetolewa kwa walengwa.
Jumamosi iliyopita, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenera Mukangara pia aliwataka wachezaji chipukizi kutojiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya wakati akitoa zawadi kwa washindi wa michuano ya BancABC SUP8R, ambapo Simba walitwaa ubingwa.

Comments