TFF YAWAOMBA RADHI WAANDISHI WA HABARI


RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF), Leodegar Tenga, amewaomba radhi waandishi wa habari kutokana na adha waliyoipata wakati wa fainali za Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hivi karibuni. 
Kutokana na tukio hilo, ambalo Waandishi walizuiwa kuingia kwenye uzio wa Uwanja huo kufanya mahojiano mara baada ya kumalizika kwa mechi ya fainali kati ya Yanga na Azam FC, ambako baadhi yao walinyanyaswa kwa namna moja ama nyingine. 
Akizungumza na Wahariri wa Michezo kwenye makao makuu ya TFF jana, Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Michezo Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, (CECAFA), alisema, yeye ni muumini wa haki, hivyo amesikitishwa na hali iliyojitokeza, hivyo anaomba radhi na asingependa hali hiyo iendelee tena. 
“Mimi ni muumini wa haki, nawaomba radhi na kuwapa pole wale waliopata misukosuko siku ile, sioni kwanini hili linajitokeza. Nikiwa Rais wa TFF na Mwenyekiti wa CECAFA nawaomba radhi, halileti ‘image’ nzuri, hata kama kulikuwa na kuna kuelekzana lakini si kwa hali hii,” alisema Tenga. 
Tenga aliwataka viongozi wa TFF, Katibu Mkuu na Ofisa Habari, kukutana na viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kukutana kujadili hali hiyo na kuweka mambo sawa ili isije tokea tena huku akisisitiza, njia ya majadiliano ndio muafaka wakati wote. 
Awali kutokana  na mtafaruku huo, TASWA ilitangaza mgogoro na kufikia uamuzi wa kususia masuala yote yanayolihusu baraza hilo.

Comments