TFF YATANGAZA TAREHE YA CHAGUZI ZA MIKOA

KAMATI ya  Uchaguzi ya Shirikisho la soka  Tanzania (TFF) imefanya mabadiliko madogo katika ratiba za uchaguzi za wanachama wake ambapo ratiba za uchaguzi za vyama wanachama wa TFF ambavyo vimekwishaanza mchakato na ambavyo havijaanza mchakato huo.
Katibu mkuu wa TFF Angetile Osiah amesema  kwamba, wamelazimika kufanya mabadiliko hayo baada ya baadhi ya wanachama wao wa mikoa kuomba iwe hivyo baada ya kubadili tarehe zao za kufanya uchaguzi.
Alisema baada ya kutokana na mabadiliko hayo,  vyama wanachama wake havinabudi kuzingatia kikamilifu ratiba  iliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na Kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF katika kutimiza wajibu wao wa kikatiba.
Osiah alizitaja tarehe hizo mpya ni pamoja na Oktoba 7 kwa mkoa wa Arusha (ARFA), Dar es Salaam (DRFA) itakayofanya Oktoba 14, Geita (GEREFA)- Novemba 10, Iringa (IRFA) - Septemba 8, Katavi - Novemba 10, Kigoma (KRFA)-Septemba Mosi, Kilimanjaro (KRFA) –Septemba 8, Lindi (LIREFA)- Oktoba 20, Manyara (MARFA)-Septemba 15, Mbeya (MREFA)-Oktoba 21, Mwanza (MZFA)-Novemba 8 na (NJOREFA)-Septemba 15.
Mingine ni Pwani (COREFA)-Oktoba 14, Rukwa (RUREFA)-Oktoba 7, Ruvuma (FARU)-Novemba 3, Shinyanga (SHIREFA)-Oktoba 20, Simiyu (SIFA)-Oktoba 27, Tabora (TAREFA)-Oktoba 6, Tanga (TREFA)-Novemba 3,Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA)-Novemba 10, Chama cha Madaktari wa Michezo  (TASMA)-Oktoba 27, Umoja wa Wanasoka ( SPUTANZA)-Oktoba 28, Waamuzi (FRAT)-Septemba 30 na  Soka ya Wanawake (TWFA)-Novemba 4.
Alisema kamati ya Uchaguzi ya TFF haitabadilisha ratiba hiyo kutokana na wilaya yoyote kutokamilisha uchaguzi wake, na hivyo kuzitaka Kamati za Uchaguzi za Mikoa kuhakikisha chaguzi zinafanyika kwa mujibu wa ratiba hiyo..
 “Kamati pia inazitaka Kamati za Uchaguzi za Mikoa kusimamia kikamilifu na kwa umakini chaguzi za wilaya zinazoendelea kwenye wilaya zilizo mikoani kwao. Ni muhimu kwa kamati kuhakikisha Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF zinafuatwa na kusimamiwa kwa umakini”, alisema .
 Osiah aliongeza kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF pia imebaini kuwa kuna Kamati za Uchaguzi za Mikoa ambazo hazikusimamia kikamilifu chaguzi za viongozi wa wilaya, kitu ambacho kinaweza kusababisha matatizo hapo baadaye hivyo kwa mara nyingine, Kamati ya Uchaguzi ya TFF inazitaka Kamati za Uchaguzi za Mikoa kuhakikisha wanaoomba kugombea uongozi kwenye wilaya, wana sifa zinazolingana na utashi wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF na Katiba.
“Wanachama ambao hawakuzingatia ratiba hiyo, hawatapewa fursa nyingine ya kubadilisha tarehe za uchaguzi na hilo litakapotokea hatua za kikanuni zitachukuliwa”, aliongeza Osiah