SUNZU ATIMKA SIMBA SC


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba, Mzambia Felix Mumba Sunzu ameondoka nchini leo kuelekea jijini Lubumbashi, DRC kuhudhuria msiba wa dada yake ambaye alifariki dunia juzi jioni nchini humo.
Dada huyo alikuwa amekwenda kumtembelea mdogo wa Sunzu, Stopila, ambaye anachezea klabu ya soka ya TP Mazembe siku sita zilizopita lakini akakumbwa na umauti kutokana na ugonjwa wa Malaria iliyopanda kichwani (Cerebral Malaria).
Uongozi wa Simba umetoa pole kwa familia ya Sunzu pamoja na kufanikisha kuondoka kwa haraka kwa mchezaji huyo ili akaungane na familia yake.
Sunzu atarejea nchini baada ya kumaliza maziko na klabu ya Simba inaomba vyombo vya habari na wadau wengine kumpa nafasi ya kuomboleza msiba huu mzito kwake binafsi, kwa familia yake na Simba.
Mola na aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi. Amen