SIMBA SASA WAMTAKA 'LIVE' MBUYU TWITE


UONGOZI wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, umesema hauna nia mbaya na beki aliyewatosa na kujisajili kwa mahasimu wao Yanga,  Mbuyu Twite, bali unataka waonane naye ana kwa ana kwanza ili kujua kilichotokea.
Hatua hiyo, inatokana na kuwepo utata juu ya mchezaji huyo mwenye asili ya DR Congo, aliyekuwa akikipiga APR ya Rwanda, kuziingiza Simba na Yanga kwenye mvutano juu ya usajili wake.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, mjumbe mmoja wa Kamati ya Utendaji ya Simba, alisema watabadili msimamo wao wa kumchukulia hatua za kisheria Twite, pindi watakapoonana naye na kujua ukweli wa kilichotokea.
Alisema Simba kupitia Mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage, ndiyo ilianza kumsainisha mkataba Twite, kabla ya siku chache Yanga kupitia kwa mjumbe wake wa Kamati ya Utendaji, Abdallah Binkleb, naye kusafiri hadi Kigali, Rwanda na kumsainisha mkataba.
Mjumbe huyo alisema baada ya Simba kubaini hilo na kuja juu, ndipo Yanga ilipowatuma watu wanaojifanya kuwa viongozi wa FC Lupopo ya DR Congo kurudisha fedha za Simba ambao walizikataa.
“Tulizikataa kwa sababu mbili kuu; kwanza hatukufanya mazungumzo na FC Lupopo ambayo ilimhamishia kwa mkopo kwenda APR; pili, hizo fedha tulimpa mchezaji na si kiongozi wa timu yoyote wala mwakilishi wake, hivyo haileti maana kupokea hela kwa mtu tusiyemjua na bila kujua kilichotokea,” alisema kiongozi huyo na kuongeza:
“Tunataka tujue ukweli hasa, kama alitekwa na kulazimishwa kusaini au ni kipi hasa kilichotokea na ndipo tutajua la kufanya, kama ni kuchukua hizo fedha na kusamehe au kuwachukulia hatua waliomrubuni.”
Hata hivyo, kumekuwepo na taarifa tofauti juu ya usajili wa mchezaji huyo kutoka kwa viongozi wa Simba, awali Rage alidai kumsajili Twite Rwanda, huku mkataba uliotolewa katika chombo kimoja cha habari jana, unaonesha mkataba huo ulisainiwa jijini Dar es Salaam.
Kiongozi mwingine wa Simba, alidai kwamba, mkataba aliousaini Twite Kigali, ulikuwa wa kawaida, lakini mkataba wa kisheria ni ule uliosainiwa Agosti mosi, 2012 jijini Dar es Saaam kwa mwanasheria wa klabu hiyo.
Yanga inaonekana kuizidi ujanja Simba katika usajili wa Twite, baada ya kumpandishia dau kutoka dola 30,000 ambazo walikubaliana na Simba na mshahara wa dola 2,500 za Marekani kwa mwezi. Yanga walikubaliana naye kumlipa dau la dola 50,000, ikiwa ni dola 20,000 zaidi ya zile za Simba, lakini mshahara unakuwa kama ule wa Simba.