SAINFIENT AMFAGILIA JERRY TEGETE


KOCHA wa Yanga Thom Saintfiet amemsifu mshambuliaji wa timu hiyo Jerryson Tegete baada ya mchezaji huyo kuifungia Yanga bao la tatu kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya African Lyon juzi.
Kwenye mchezo huo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na Yanga kushinda kwa mabao 4-0, Tegete aliingia kipindi cha pili na kufunga bao la tatu baada ya kutumia vyema krosi nzuri ya Idrisa Rashidi kutoka upande wa kushoto.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo Saintfiet alimsifu Tegete kwa kuonyesha kiwango kizuri na kufunga bao hilo mara baada ya kuingia.
“Hakuwa kwenye kiwango bora kwenye mashindano ya kombe la Kagame, lakini amekuwa akifanya juhudi kubwa mazoezini, amecheza vizuri leo(juzi), nina furaha sana kwa yeye kucheza vizuri,”alisema Saintfiet.
Aidha, alisifu kiwango kilichoonyeshwa na timu nzima na kusema kuwa walicheza kwa nidhamu kubwa kiasi cha kutoruhusu bao kwenye lango lao.
“Kama timu inashinda bila yenyewe kuruhusu bao basi hicho ni kiwango bora, walicheza kwa nidhamu ya hali ya juu, siku zote nataka washinde bila kuruhusu bao,”alisema Saintfiet.
Alisema amefanya mabadiliko makubwa kipindi cha pili ili kujua uwezo wa kila mchezaji na hasa ukichukulia baadhi ya nyota hawakuwa na timu hiyo toka alipopewa jukumu la kuionoa Yanga.
Simon Msuva,Frank Domayo na Omega Seme walikuwa wakitumikia timu za taifa(Taifa Stars) na ile ya chini ya umri wa miaka 20(Ngorongoro Heroes). Wote waliingia kipindi cha pili kwenye mechi hiyo.