RASMI:NGASSA AKUBALI KUITUMIKIA SIMBA SC


MSHAMBULIAJI Mrisho Ngasa aliyepelekwa kwa mkopo katika klabu ya Simba akitokea Azam aliyojiunga nayo msimu wa 2009/10 akitokea Yanga, jana alisaini rasmi mkataba wa kukipiga Msimbazi.
Kwa mujibu wa habari zilizotufikia , nyota huyo aliyewahi kuichezea Kagera Stars, amepewa gari.
Mbali ya gari la kutembelea, pia Ngasa mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pamba FC ya Mwanza, Halfan Ngasa, atakuwa analipwa mshahara wa sh 2,000,000 kwa mwezi.
Kiasi hicho cha mshahara, ni kama alichokuwa akilipwa na klabu yake ya
Azam iliyomtoa kwa mkopo baada ya kukerwa na kitendo chake cha kuonesha mapenzi yake kwa timu yake ya zamani ya Yanga.
Baada ya mechi ya nusu fainali ya Kombe la Kagame dhidi ya AS Vita ya DR Congo ambapo Ngasa alifunga bao moja  kati ya 2-1, aliamua kuvaa jezi ya Yanga.
Kitendo hicho kimetafsiriwa kama mchezaji huyo kukosa mapenzi ya dhati kwa timu yake ya Azam, hivyo kumtoa kwa mkopo.
Licha ya kuwaniwa na klabu za Simba na Yanga, nyota huyo ametua Msimbazi baada ya kutoa dau la sh mil. 25, wakiipiku Yanga waliokuwa na ofa ya sh mil. 20.   
Mapema jana, Meneja wa Azam, Patrick Kahemele, alikana habari kuwa Ngasa hakuwa ameshirikishwa kwenye mpango wa kutolewa kwa mkopo.
Alisema, Ngasa alijulishwa hilo na awali, bei yake ilikuwa dola 50,000 za Marekani, ingawa baadaye ilipungua hadi sh mil. 25.
 “Tunaomba ifahamike bayana kuwa Ngasa alipewa taarifa ya kuuzwa na aliombwa asaidie kushawishi klabu anayoitaka ifike kwetu na ofa yake.
“Ngasa alitamka bayana kuwa yupo tayari kwenda klabu yoyote ambayo Azam ingeona imekidhi mahitaji yake kwa masharti kuwa masilahi yake ya kimkataba kati yake na Azam yazingatiwe,” alisema na kusisitiza:
“ Kwa maana hiyo, Azam iliamua kumpeleka Ngasa kwa mkopo kwa klabu iliyofika na kuonesha nia ya kumhitaji (Simba), ikipewa sharti la kumlipa Ngasa mshahara wake kamili (sh 2,000,000) pamoja na stahiki zake nyingine zote
za kimkataba,” alisema.
Aliongeza kuwa, kama Ngasa anataka kuvunja mkataba wake au kama Yanga bado wanamhitaji, watoe dola 50,000,
kwani nyota huyo bado ni mali ya Azam.
Kahemele alisema kama Ngasa akiamua kubaki Azam, atakaa nje ya uwanja kwa muda wote uliosalia kwenye mkataba, kwani hawapo tayari kumvisha jezi yao.
Mbali ya klabu ya Azam kumwadhibu Ngasa kwa kumtoa kwa mkopo kwa kosa la kuvaa jezi ya Yanga, pia imemtimua aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Stewart Hall.
Hall ametupiwa virago baada ya kukaidi agizo la kutakiwa kutompanga Ngasa katika mechi ya fainali ya Kombe la Kagame dhidi ya Yanga.
Katika mechi hiyo ambayo iliisha kwa Yanga kushinda mabao 2-0, Hall alimwingiza Ngasa badala ya Kipre Tchetche.