POULSEN AANZA KUWAPIKA WASHAMBULIAJI WAPYA STARS


Kocha wa Stars, Kim Poulsen

Na Mwandishi Maalumu, Gaborone, Botswana 
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Kim Poulsen ameanza kazi ya kutengeza washambuliaji wapya katika kikosi chake huku akianza na Haruna Moshi ‘Boban’.
Kocha huyo ameamuwa kutengeneza safu ya washambuliaji ili timu hiyo iweze kuwa na hazina ya washambuliaji wenye uchu wa kupachika mabao.
Stars ambayo inadhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager inajiandaa kucheza mechi za kuwania kufuzi nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2018.
Akizungumza na Boban jana (juzi) usiku baada ya mazoezi ya timu  hiyo hapa mjini Gaborone nchini Botswana  Poulsen alisema “Wewe ni mchezaji mzuri sana na una uwezo mkubwa wa kuisaidia timu, na kuanzia leo ninakupa jukumu la kucheza kama mshambuliaji na si kiungo mshambuliaji”alisema Poulsen na kuongeza:
“Nakupa kazi hii kwa sababu nimegundua kuwa ukicheza kama mshambuliaji unaweza kufunga magoli mengi kuliko ukicheza kama kiungo, sababu ya msingi ni kwamba ninataka uzibe pengo lililoanza kujitokeza hivi sasa, baada ya Mbwana Samatta,Thomas Ulimwengu,na John Bocco kukosekana”.
Katika mazungumzo ya kocha huyo yaliyodumu kwa zaidi ya dakika 15 baada ya mazoezi, Poulsen aliendelea kumwambia Boban kwamba, “katika kikosi changu wewe ndiyo mchezaji mwenye uzoefu mkubwa kuliko wote na nimegundua kwamba hata wachezaji pia wanakuheshimu na mnashirikiana vizuri, ndani na nje ya uwanja mbali na hilo wewe ni kati ya wachezaji wanaotambua wajibu wao ndani na nje ya Uwanja,sawa Moshi”.
Baada ya Poulsen kuzungumza na Boban alisema kwamba kuanzia sasa Boban atakuwa akicheza kama mshambuliaji katika timu hiyo na si kama kiungo mshambuliaji.
Alisema Boban ni mchezaji mwenye akili sana na asiye na papara anapokuwa ndani ya eneo la kufunga na kwamba ni kati wachezaji wachache wanaocheza nafasi ya kiungo wenye uwezo wa kufunga.
Akielezea sifa za Boban Poulsen alisema kwanza sifa ya mshambuliaji mzuri ni yule asiyekuwa na ubinafsi kwamba lazima afunge yeye,na Boban ana sifa hiyo, Boban sio mchoyo wa kutoa pasi anapoona kwamba hawezi kuendelea kukaa na mpira wakati kuna mtu mwingine ana nafasi lazima atoe pasi.
“Ukiwa na mchezaji kama huyu pale mbele nilazima upate ushindi kwa sababu mabeki watakuwa akimlinda sana yeye wakijua kwamba atafunga yeye kumbe anatoa pasi kwa mfungaji mwingine, na hilo ndiyo tatizo la wachezaji watanzania, kwani hawachezi kitimu mshambuliaji anajuwa kuwa yeye ndiyo mwenye jukumu la kufunga peke yake kumbe sivyo”.
Akizungumza vitu vichache ambavyo anapaswa kumpatia Boban ili aweze kumudu nafasi hiyo vizuri Poulsen alisema kuwa ni pamoja na kujitambua kuwa yeye sasa ni mshambuliaji na si kiungo, kuongeza uwezo wa kujiamini kwamba anaweza kukabiliana na beki wa aina yeyote,kuongeza kasi na kufanya maamuzi ya haraka, na kuwahamasisha wenzake kuwa kila kitu kinawezekana hasa pale anapofanikiwa kufunga goli.
Katika hatua nyingine alisema kwamba timu iko vizuri na hakuna majeruhi hata moja  na kwamba hana wasiwasi wowote juu ya mechi hiyo.
Kwa upande wake Boban alisema kwamba amekubaliana na uwamuzi wa Mwalimu kwa sababu amegundua kwamba akicheza kama mshambuliaji ataisaidia timu zaidi kuliko akicheza kama kiungo hivyo yeye kama mchezaji hana tatizo na atafuata ushauri wa mwalimu.
“Mimi sina tatizo kwakuwa Kocha mwenyewe ndo ameona hivyo basi mimi sioni ugumu wowote kwa sababu najua kufunga na lengo ni kuisaidia timu yetu ipate ushindi.



Comments

Post a Comment