OKWI AENDELEA KUBAKI UGANDA


NYOTA wa kimataifa wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi ataendelea kubaki kwao Uganda baada ya Shirikisho la Soka la nchi hiyo, FUFA, kuwaandikia Wekundu wa Msimbazi, barua kumuomba aendelee kuwepo huko.
Awali, Okwi ambaye alikuwa kwao kuitumikia timu ya taifa, The Cranes katika mechi yao ya kirafiki ya kalenda ya FIFA dhidi ya Malawi, ilikuwa arejee nchini Jumapili kujiunga na wenzake waliopo kambini jijini Arusha.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba, FUFA imemtaka Okwi aendelee kubaki Uganda na wenzake, kwani wanatarajia kucheza na Botswana Agosti 26.
Alisema, mbali ya Okwi, mchezaji mwingine wa kimataifa wa timu hiyo, Mussa Mude, pia wa Uganda ambaye alikuwa majeruhi, hali yake imetengemaa na kufikia mwisho wa mwezi huu, atakuwa ameshajiunga na wenzake.
Katika hatua nyingine, Kamwaga alisema kutokana na kusogezwa mbele kwa Ligi Kuu bara, Simba itaendelea kujichimbia Arusha hadi Septemba 8 itakaporejea jijini Dar es Salam kwa ajili ya mechi yake ya kuwania Ngao ya Hisani dhidi ya Azam FC.