NGORONGORO HEROES YATUA SALAMA NIGERIA


Ngorongoro Heroes, timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 imewasili asubuhi hii (Agosti 10 mwaka huu) kwa ndege ya Overland Airways kwenye mji wa Ilorin, Jimbo la Kwara lililo Kusini mwa Nigeria tayari kwa mechi ya marudiano dhidi ya wenyeji Flying Eagles itakayochezwa Jumapili. 
Mechi hiyo ya raundi ya pili ya michuano ya U20 ya Afrika itachezwa kwenye Uwanja wa Township kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa hapa ambapo Tanzania itakuwa ni saa 12 kamili jioni. Ngorongoro Heroes ilitua jana (Agosti 9 mwaka huu) jijini Lagos ambapo ililala kabla ya kuja hapa. 
Msafara wa Ngorongoro Heroes wenye watu 27 ukiongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA) ulipokea na Ofisa Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria, Jones Mndeme na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF) umefikia hoteli ya Kingstone Grand Suites. 
Kwa mujibu wa Kocha wa Ngorongoro Heroes, Jakob Michelsen, timu itafanya mazoezi leo jioni (Agosti 10 mwaka huu) wakati mazoezi ya mwisho yatakuwa kesho jioni (Agosti 11 mwaka huu) kwenye uwanja ambao utatumika kwa mechi ya Jumapili. 
Wachezaji wote wako katika hali nzuri isipokuwa Issa Rashid na Aishi Manula ambao walikuwa wakisumbuliwa na tumbo baada ya timu kufika jana (Agosti 9 mwaka huu) jijini Nairobi, Kenya ambapo ilibadili ndege kuja Nigeria. Hata hivyo, hali zao zinaendelea vizuri na huenda wakawa sehemu ya kikosi cha kwanza kitakachoivaa Flying Eagles. 
Mbali ya Rashid na Manula, wachezaji wengine walioko hapa kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes ni Barwany Khomeiny, Samir Ruhava, Dizana Yarouk, Leonard Muyinga, Hassan Ramadhan, Jamal Mroki, Omari Kheri, Frank Domayo, nahodha Omega Seme, Abdallah Kilala, Hassan Dilunga, Ramadhan Singano, Simon Msuva, Said Zege, Atupele Gren na Ramadhan Salum. 
Mbali ya Michelsen, Benchi la Ufundi linaundwa na Mohamed Rishad 'Adolf' (Kocha Msaidizi), Peter Manyika (Kocha wa makipa), Nassoro Matuzya (Daktari), Joakim Mshanga (Physio), Juma Kizwezwe (Mtunza vifaa) na Meneja wa timu John Lyimo. 
Flying Eagles ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 2-1 nayo tayari imeshaingia hapa Ilorin ikitokea Lagos kwa mechi hiyo ambayo matokeo yake yataamua timu ipi itaingia raundi ya tatu ambayo ni ya mwisho kabla ya fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazofanyika mwakani nchini Algeria. Timu itakayovuka itacheza raundi hiyo na mshindi kati ya Congo Brazzavile na Afrika Kusini.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Ilorin, Kwara State, Nigeria
+2347068557566

Comments