NGASSA AACHA GUMZO BOTSWANA


Na Mwandishi Maalumu, Gaborone
MSHAMBULIAJI wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Mrisho Ngassa, ameacha gumzo jijini hapa baada ya kuwa mwiba mkali kwa safu ya ulinzi ya Botswana ‘Zebras’ katika moja kati ya mechi kadhaa za kirafiki za kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), zilizochezwa juzi, siku.
Katika pambano hilo, Ngassa alifanikiwa kuiongoza Stars kupata matokeo ya sare ya mabao 3-3 katika mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Molopolole.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, ilikuwa ikishangiliwa na watanzania zaidi ya 100 wanaoishi nchini Botswana, huku wakiwa na bendera ya Taifa.
Mashabiki wa soka mjini hapa, walianza kulitambua jina la Ngassa baada ya kufanikiwa kuwatoka mabeki wa Zebras, kabla ya kipa wa timu hiyo Mompolok Sephekolo kumchezea rafu ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kuamuru ipigwe penalti, iliyofungwa kwa ustadi mkubwa na beki Erasto Nyoni dakika ya 18.
Baada ya bao hilo, Botswana walianza kulishambulia lango la Stars kama nyuki na dakika ya 25,  mshambuliaji Lemponye Tshireletjo alisawazisha, baada ya mabeki wa Stars kushindwa kuokoa mpira uliopigwa kutoka upande wa kushoto na kumkuta aliyeunganisha mpira wavuni, huku kipa Juma Kaseja akishindwa kufanya kazi yake ipasavyo.
Hata hivyo, baada ya wanyeji kupata bao la kusawazisha, kiungo Mwinyi Kazimoto akaifungia Stars bao la pili dakika ya 31 kwa shuti kali la mita takribani 30.
Kazimoto, alifunga bao hilo baada kipa wa Zebras, Sephekolo kushindwa kudaka shuti la Ngassa alilookoa kwa mguu na mpira kumkuta mfungaji.
Mbali ya kazi kubwa iliyokuwa ikifanywa na Ngassa kwa kushirikiana vizuri na Haruna Moshi ‘Boban’ pamoja na Said Bahanuzi na kufunikiwa kucheka na nyavu, safu ya ulinzi iliruhusu mabao kuingia nyavuni kirahisi.
Hali hiyo, iliendelea dakika ya 37 ikiwa ni dakika 6 tu tangu Kazimoto alipofunga bao la kuongoza, mshambuliaji mahiri wa Zebras, Tshireletjo alipachika bao lake la pili na la kusawazisha, baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa kutoka pembeni mwa
uwanja na kumshinda Kaseja na kufanya matokeo kuwa 2-2 hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.
Kipindi cha pili, timu zote ziliingia uwanjani zikiwa na lengo la kupata mabao ya kuongoza, huku Botswana ikiwa ya kwanza kupata bao lililofungwa kwa kichwa tena na Tshireletjo dakika ya 70.
Stars, ilipata pigo dakika 80, baada ya beki Erasto Nyoni kulimwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mshambuliaji wa Botswana, huvyo kumlazimisha Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kim Poulsen, kufanya mabadiliko ya kumtoa Boban na Bahanuzi na nafasi zao kuchukuliwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ na Simon Msuva.
Mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa Stars huku Msuva akishirikiana vema na Ngasa na katika dakika ya 90, Msuva alifanya kazi ya kuwatoka mabeki wa Botswana kabla ya kutoa pasi ya mwisho kwa Ngassa aliyetupia mpira kambani na kubadili matokeo kuwa 3-3.
Akizungumzia matokeo hayo, Kocha Poulsen alisema kuwa, timu yake ilicheza vizuri isipokuwa safu ya ulinzi ndio haikufanya kazi yake ipasavyo.
“Nikweli kabisa kwamba, beki haikucheza vizuri, kwani waliwachosha washambuliaji wangu, haina maana ya kufunga mabao kisha yanarudi, inatia hasira kuona mabao yanafungwa kirahisi ndani ya dakika chake, yaani sisi tunafunga mabao ya shida lakini wao wanafunga mabao mepesi, hivyo nitayafanyia kazi mapungufu hayo kabla ya mechi inayofuata," alisema Poulsen.
Stars imerejea jijini jana usiku.

Comments