MPIGANAJI CYPRIAN MUSIBA 'AKA'MZEE WA MWIBARA AJITOSA KUWANIA UJUMBE NEC YA CCM


ALIYEKUWA mwandishi  Mwandamizi wa Televisheni ya Channel Ten, Cyprian Musiba (34), amechukuwa fomu ya kugombea nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa (NEC), na Mkutano Mkuu wa chama hicho ngazi ya taifa wilayani Bunda mkoani Mara.
Musiba ambaye amechukua fomu hizo juzi mchana na kuzirudisha jana asubuhi Makao Makuu ya Ofisi ya CCM Bunda, amesema dhamira yake ya kuomba nafasi hizo mbili ni kwenda kukijenga chama katika nyanja zote
za kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Alisema atapambana kwa nguvu zake zote kudhibiti rushwa, siasa za chuki, fitna na makundi ndani ya chama chake hicho tawala.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukuwa fomu hizo, Musiba alisema moja ya mambo yanayokichafua chama chake mbele ya umma wa Watanzania, ni vitendo vya rushwa, siasa chafu yakiwemo makundi na fitna.
Musiba alimuomba Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah kuwapanga vema makamanda wake kwa ajili ya kuwakamata wagombea na watu watakaobainika kutoa rushwa ili wachaguliwe kwenye ngwe hiyo ya kuwania uongozi.
"Nimechukua fomu hii kwa lengo la kwenda kupigania maendeleo ya
chama changu tawala. Nitapambana kuhakikisha rushwa, siasa chafu ndani ya CCM vinaondoka, maana ndiyo vitu vinavyokiharibu kabisa chama.
"Kwa maana hiyo, kuanzia sasa naiomba TAKUKURU ianze kuwafuatilia na kuwakamata wagombea wote watakaoonekana kutoa rushwa
wakati huu wa uchaguzi," alisema Musiba.
Musiba ni miongoni mwa wanachama 13 waliochukuwa fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya U-NEC kupitia wilaya hiyo.