JULIO AFAGILIA CHUJI KUREJESHWA STARS


KOCHA Msaidizi wa timu za taifa za vijana, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amepongeza kurejeshwa katika kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kiungo wa Yanga, Athuman Iddi ‘Chuji’.
Kocha Mkuu wa Stars, inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro, Mdenish Kim Poulsen, juzi alitangaza majina ya nyota 21, akiwamo Chuji ambaye kwa mara ya mwisho aliitwa katika kikosi hicho mwaka 2010, kikiwa chini ya Mbrazil, Marcio Maximo.
Julio alisema, kurejeshwa kundini kwa Chuji kunatokana na jitihada zake binafsi, ambazo amekuwa akizionyesha katika timu yake ya Yanga.
Alisema Chuji ni mchezaji mzuri, mwenye kipaji na anayejituma uwanjani, lakini kipindi cha katikati alighafirika na matokeo yake kupoteza mwelekeo, lakini baada ya kuwekwa chini alizinduka.
“Ni nani asiyekubali kiwango alichokionyesha Chuji katika siku za hivi karibuni na hata ubingwa wa Kagame kwa Yanga na yeye alichangia pia kwa jitihada zake,” alisema.
Julio aliongeza kuwa uwepo wa Chuji Stars utasaidia kwa kiasi kikubwa, kwani ni mchezaji mzoefu, hivyo atakaposhirikiana na wenzake timu inaweza kupata mafanikio makubwa.
Hali kadhalika, Julio alipongeza uteuzi huo wa kikosi cha Stars, ambacho kitaingia kambini Agosti 8 kwenye Hoteli ya Tansoma kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya kimataifa ya kirafiki itakayopigwa ugenini Agosti 15.
Alisema kocha amefanya jambo la maana, kuchanganya damu changa na wakongwe, hali itakayoleta changamoto kubwa uwanjani.
Mbali na Chuji, wengine ni makipa Deogratias Munishi, nahodha Juma Kaseja na Mwadini Ali. Mabeki ni nahodha msaidizi, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani na Shomari Kapombe, huku viungo ni Frank Domayo, Haruna Moshi, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Chombo, Ramadhan Singano, Salum Abubakar na Shabani Nditi.
 Washambuliaji ni John Bocco, Mbwana Samata, Said Bahanuzi, Simon Msuva na Thomas Ulimwengu.

Comments