JKT RUVU MABINGWA LIGI YA MAJESHI


TIMU ya soka ya JKT Ruvu jana imefanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi maalum wa timu za majeshi zinazorajiwa kushiriki ligi kuu soka Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 iliyokuwa ikifanyika kwenye uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi, Pwani. 
JKT ilitwaa ubingwa huo kutokana na kufikisha pointi 9 ilizozipata kupitia michezo yake mitano ya ligi hiyo iliyoanza kutimua vumbi Agosti 15 mwaka huu na kushirikisha timu 6. 
Kwa ushindi huo, maafande hao walikabidhiwa kombe kubwa pamoja na fedha taslimu sh 100,000 kutoka kwa mgeni rasmi katika fainali hizo Hassan Othman ‘Hassanoo’ ambaye ni mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Pwani (COREFA). 
Oljoro JKT ilishika nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 9 pia, Mgambo ilishika nafasi ya tatu kwa pointi sita, Ruvu Shooting ilishika nafasi ya nne kwa kuwa na pointi sita, wakati polisi Dar es Salaam ilishika nafasi ya  tano kwa pointi sita na African Lyon ambayo ilikuwa timu mwalikwa ilishika mkia kwa kuwa na pointi tatu. 
Mshambuliaji wa maafande wa JKT Oljoro Paul Nonga aliibuka kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo.