HATMA YA WACHEZAJI WATAKAOACHWA SIMBA SC MIKONONI MWA RAGE


Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
WAKATI mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania Bara, Simba wakipanga kumuuza nyota wake wa Zambia kwa dau la walau hata dola.20,000  hatma ya wachezaji watakaoichezea timu hiyo katika msimu ujao wa ligi na michuano ya kimtaifa ipo mikononi mwa kamati ya utendaji ya klabu hiyo. 
Aidha, uwezekano wa kumuacha nyota wake Salim Kinje iliyemsajili kutoka klabu ya AFC Leopards ni mdogo, huku mshambuliaji wake wa kimataifa Kanu Mbiyavanga akikalia kutu kavu kutokana na kucheza mpira wa kufuata kelele za jukwaani. 
Habari za uhakika toka klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Msimbazi zinaeleza kwamba kamati ya utendaji ya klabu hiyo imeitisha kikao cha dharura kwa ajili ya kujadili mustakabali mzima wa wachezaji wa timu hiyo. 
Kiongozi mmoja wa kamati ya utendaji aliliambia Tanzania Daima jana kwamba kikao hicho kitafanyika wakati wowote katika siku mbili hizi ambapo wanasubiri ujio wa Mwenyekiti wao Alhaj Ismail Aden Rage ambaye yupo Dodoma akihudhuria vikao vya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Alisema kikao hicho kitajadili mapendekezo ya kamati ya ufundi ya klabu hiyo iliyowasilishwa mezani na ndipo yatakapotolewa maamuzi na nani ataichezea Simba, nani ataachwa na nani atauzwa au kupelekwa kwa mkopo.
Kiongozi huyo alisema Sunzu ambaye klabu ya Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeonyesha nia ya kutaka kumnunua hawatosita kufanya hivyo kwani kwa sasa kiwango chake hakikidhi mahitaji ya klabu hiyo. 
“Suala la Sunzu kidogo lina ugumu kwani bado ana mkataba na Simba sasa kama tutaamua kumuacha (kuvunja mkataba) itabidi tumlipe fedha nyingi ndiyo maana tunaona tumuuze hata kwa dola 20,000,”alisema kiongozi huyo. 
Kuhusiana na Kinje, kiongozi huyo alisema bado ananafasi ya kuitumikia timu hiyo kwani ni mchezaji mzuri isipokuwa hajachezeshwa katika nafasi anazozimudu  ambazo ni namba nne na tano. 
“Pia kuna wachezaji kama Lino Masombo, Haruna Shamte hawana nao walipendekezwa kuondolewa sasa tutakapokutana tutajua zaidi maana ni muhimu kuangalia ni nani anaisaidia timu na nani mzigo”,aliongeza .