YANGA WAPELEKA 'CHEKECHEA ' ZENJI


BAADA ya awali kugoma kushiriki michuano ya kombe la Urafiki inayoendelea Visiwani Zanzibar, uongozi wa timu hiyo umeamua kupeleka kikosi chake cha pili.
Awali Yanga waligoma kushiriki michuano hiyo kwa hoja ya kuhofia majeruhi kuelekea michuano ya Kagame, juzi jioni walithibitisha ushiriki wao ambapo leo itashuka dimbani kukwaana na Jamhuri ya Pemba.
Ofisa habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema mapema jana mchana kuwa, kikosi kingeondoka jioni ya jana.
Hata hivyo, Sendeu alidai pia kikosi cha Yanga kingefanya mazoezi jioni ya jana kwenye Uwanja wa Kaunda akiwemo Niyonzima aliyetua akitokea kwao Rwanda.
Kauli hizo mbili tofauti za Sendeu, zilionekana kuleta utata na alipobanwa juu ya timu ipi ingekwenda Zanzibar na ipi ingebaki Kaunda, akaonekana kubabaika kabla ya kusema apigiwe simu baadaye.
Yanga, mabingwa watetezi wa michuano ya Kagame wataanza kampeni Julai 14 dhidi ya Atletico ya Burundi katika kundi C, huku Simba wakianza na URA ya Uganda.