YANGA, MAFUNZO KUMENYANA LEO ROBO FAINALI KAGAME


 Yanga Sc
Mafunzo SC

MABINGWA watetezi wa Kombe la Kagame, Yanga, leo wanawakabili Mafunzo ya Zanzibar katika mechi ya robo fainali itakayochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijiji Dar es Salaam.
Yanga iliyomaliza nafasi ya pili katika kundi la C, itakuwa na kibarua kigumu cha kuwatupa nje ya michuano hiyo Mafunzo kama wanataka kutinga nusu fainali.
Mechi hiyo itakayoanza majira ya saa 10 ikitanguliwa na mechi kati URA ya Uganda na APR ya Rwanda ambao watakumbana kuanzia majira ya saa 8.  
Wakati Mafunzo wakitaka kudhihirisha umahiri wao uliowapa wakati mgumu mabingwa wa Kenya, Tusker, Yanga wamekamia kutinga nusu fainali.
Yanga watawakabili Mafunzo wakitoka kuvuna ushindi wa 2-0 dhidi ya APR katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi.
Mechi nyingine leo itakuwa kati ya URA, iliyomaliza hatua ya makundi ikiwa na pointi 9, baada ya kushinda mechi zote tatu.
Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet alisema juzi, kikosi chake kitapambana kushinda ili kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.
Alisema, kwa kiwango kilichooneshwa na vijana wake katika mechi ya tatu dhidi ya APR, hana shaka na uwezo wa timu yake kufika fainali.
“Licha ya kuanza vibaya michuano hii, tuliketi chini kufanyia kazi dosari, ndio maana timu imeanza kubadilika, sina wasiwasi na mechi ya robo fainali,” alisema.