YANGA, AZAM FC VITANI LEO


MECHI mbili za nusu fainali ya michuano ya Kombe la Kagame, zinapigwa leo huku mabingwa watetezi, Yanga wakikabiliwa na kibarua kigumu cha kuwang’oa maafande wa APR ya Rwanda, mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Hiyo itakuwa nusu fainali ya pili, baada ya kuwashuhudia waalikwa AS Vita ya DR Congo iliyowatupa nje ya michuano hiyo Atletico ya Burundi wakikwaana dhidi ya Azam FC, inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
Yanga chini ya Kocha Mkuu Mbelgiji Tom Sainfiet, itakutana na APR ikiwa ni siku chache tangu wakutane kwenye mechi ya mwisho ya hatua ya makundi na wakali hao wa Jangwani kushinda mabao 2-0.
Hata hivyo, Yanga hawapaswi kubweteka kwani timu hizo zilikutana huku zote zikiwa na tiketi ya robo fainali, hivyo ilikuwa ni mechi ya kukamilisha ratiba hadi Warwanda hao kupumzisha nyota wake kadhaa.
Yanga ambao msimu ujao hawatacheza michuano ya kimataifa baada ya kumaliza msimu uliopita wakiwa nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Azam, watakuwa na kazi ya kupigania ushindi na hatimaye kutetea taji hilo.
Wakati Yanga wakitaka kushinda mechi ya leo na hatimaye kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya tano, APR wanataka kuubeba kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitano.
Yanga ikibeba taji hilo mwaka 1975, 1993, 1999 na 2011, APR wana rekodi ya kujitwisha mara mbili, 2004 na 2007.
Aidha, wakati Yanga ikitinga hatua hiyo baada ya kuwang’oa mabingwa wa soka wa Zanzibar, Mafunzo kwa penalti 5-3, APR iliwafungasha virago URA ya Uganda kwa mabao 2-1.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka (TFF), Boniface Wambura, kiingilio cha kushuhudia mechi za leo kitakuwa shilingi 5,000; 7,000; 15,000 na 20,000.    
Alisema, mechi ya kwanza kati ya Azam na AS Vita, itaanza majira ya saa 8 kamili mchana kabla ya Yanga kuwakabili maafande wa APR itakayoanza saa 10 jioni.

Comments