WAGOMBEA SABA YANGA WATAKIWA KUWASILISHA VYETI VYA SEKONDARI, KAMPENI KUANZA IJUMAA


WAKATI kampeni kwa wanaowania uongozi katika klabu ya soka ya Yanga zikitarajiwa kuanza ijumaa,  kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo imewataka baadhi ya wagombea kuwasilisha nakala halisi ya vyeti vyao vya sekondari.
 Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Yanga, Jaji mstaafu John Mkwawa alisema kwamba mwisho wa kuwasilisha vyeti hivyo ni  kesho na baada ya hapo ndipo wataendelea na taratibu nyingine za uchaguzi. 
Jaji Mkwawa aliwataja wagombea hao ni pamoja na Sarah Ramadhan anayewania nafasi ya uenyekiti, Clement Sanga (Makamu Mwenyekiti, Edger Fongo, Ramadhan Kampira, Mohammed Mbaraka, Abdallah Binkleb na Omary Ndula. 
“Kamati inawaagiza wagombea hawa kuwakilisha nakala zao halisi za vyeti vya sokendari mpaka kufikia kesho (leo), hivyo kamati inasisitiza hilo ili tuweze kuendelea na hatua zinazofuata,”alisema. 
Uchaguzi mdogo wa viongozi wa Yanga unatarajiwa kufanyika Julai 15 mwaka huu katika ukumbi utakaotangazwa baadaye ambapo nafasi za mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wanne wa kamati ya utendaji zitajazwa. 
Wagombea waliokidhi vigezo mpaka sasa ni pamoja na Jonh Paul Jambele, Yusuf Manji na Edgar W. Chibula wanaowania Uenyekiti, Ayoub Nyenze na Yono Stanley Kevela.wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti, huku Jumanne Mwamenywa, Beda Tindwa,Ramadhan Said,Shaban Katwila na Lameck Nyambaya wakiwania ujumbe. 
Wengine ni Peter H. Haule,   Justine S. Baruti Yono Kevela, Mosess K. Valentino, Aaron Nyanda, George M. Manyama,Abdalah Sharia Ameir,Jamal  Kisongo na Gaudiusus Ishengoma ambao pia wanawania nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji.