WADAU WAOMBWA KUUNGA MKONO KAMPENI YA KULIPAMBA TAIFA NA SANAA ZA NYUMBANI


 Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Adrian Nyangamalle (Kulia) akisisitiza jambo kwenye mwendelezo wa vikao vya maandalizi ya kampeni ya kulipamba taifa na Sanaa za nyumbani vinavyofanyika Ukumbi wa BASATA. Katikati ni Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego na Katibu wa shirikisho hilo Godfrey Ndimbo.
 Katibu Mtendaji wa BASATA Bw. Materego akiongea na wajumbe wa Kamati ya kundaa kampeni ya Kulipamba taifa na Sanaa za nyumbani (hawako pichani) inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Mmoja wa wajumbe wa kamati ya Kulipamba taifa na Sanaa za nyumbani Fred Halla

Na Mwandishi Wetu

Wadau mbalimbali nchini hususani viongozi wa kitaifa na kidini, wanasiasa na wamiliki wa majengo mbalimbali nchini wameombwa kuunga mkono kampeni ya kulipamba taifa na kazi za Sanaa za kitanzaia inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Akizungumza katikati ya wiki hii kwenye mwendelezo wa vikao vya maandalizi ya kampeni hiyo Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi nchini Adrian Nyangamalle alisema kuwa uungwaji mkono wa wadau hao utalifanya taifa kupendeza na kuwa kivutio kwa kila mtu.

“Tunategemea kwa kiwango kikubwa uungwaji mkono kutoka kwa wadau hasa viongozi wetu wa kitaifa, lengo ni kumfanya kila mtanzania aone fahari kwa kupamba na Sanaa za nyumbani lakini pia afurahie mandhari nzuri ya taifa lake” alisema Nyangamalle.

Kwa mujibu wa Nyangamalle, Tanzania imejaaliwa Sanaa nyingi za mikono kama za vinyago na michoro, zina mvuto wa aina yake, zinavuta wageni wengi kuja kuzitazama hivyo kuzipamba kwenye maeneo yetu ya wazi na maofisi kutabadili kabisa muonekano wa miji na ofisi zetu.

“Tunalenga kampeni hii isambae, ifike mahali iwe lazima kwa ofisi zetu za umma na maeneo ya wazi kupambwa na Sanaa za mikono kutoka nyumbani. Ni wazi viongozi wetu wakiunga mkono tutaleta mabadiliko” alisisitiza Nyangamalle.

Kuhusu mikakati ya uzinduzi wa kampeni hiyo Rais huyo mwenye dhamana na Sanaa za mikono nchini alisema kuwa, inaendelea vizuri na kwa hatua za mwanzo itahusisha maonesho ya Sanaa za kupamba maofisini sambamba na kushawishi watendaji maofisini kununua kazi hizo za mikono.

“Bado hatujapanga kalenda rasmi ya uzinduzi wa kampeni hii lakini mikakati inaendelea vizuri, wito wangu ni kuomba viongozi wetu wa juu na watanzania kuona umuhimu wa kampeni hii” alimalizia Nyangamalle.
 

Comments