VODACOM YAJIVUNI UDHAMINI WAKE LIGI KUU TANZANIA BARA


Mkuu wa masoko na mawasiliano wa Vodacom, Kelvin Twisa

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom imejivunia udhamini wake kwa ligi kuu soka Tanzania bara na kusema umeleta manufaa makubwa katika maendeleo ya mchezo huyo.
Akizungumza juzi katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa ligi hiyo,  mkuu wa masoko  na mawasiliano wa Vodacom Kelvin Twisa alisema kampuni yake imetoa zaidi ya shilingi milioni 113 kama zawadi za washindi hao na hivyo kufanya mwaka huu zwadi kuongezeka tofauti na mwaka jana zilikuwa shilingi milioni 90.8.
“Tunajivunia kuwa wadhamini wa ligi kuu bara ambapo vipaji vingi vimeonekana na viwango vya kuvutia pia katika mechi zote na ndio maana hii leo tupo katika kutoa zawadi kwa washindi,”alisema.
Katika halfa hiyo, ilitambulishwa tuzo mpya inayohusisha wachezaji vijana waliofanya vema kwenye timu hizo ambapo waliotwaa ni pamoja na Rashid Mandawa (Coastal Union), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting) na Frank Damayo aliyekuwa anaichezea JKT Ruvu na sasa amesajiliwa Yanga ambapo kila mmoja alizawadiwa shilingi milioni moja.
Azam Fc ilifanikiwa kuongoza kwa kutwaa tuzo tano ikiwemo ile ya nafasi ya pili iliyowapatia sh.mil.22, timu yenye nidhamu (mil.7.8), kocha bora-Stewart Hall (mil.3.8), mfungaji bora- John Bocco (mil.3.9) na mchezaji bora- Aggrey Morris (mil.3.3).
Aidha mabingwa Simba walitwaa mil.50, huku kipa wake Juma Kaseja alitwaa tuzo ya kipa bora na kuzawadiwa Mil.3.3, wakati Yanga ilizawadiwa mil.15 kwa kushika nafasi ya tatu na Martin Sanya alitwaa tuzo ya mwamuzi bora na kuzawadiwa mil.3.8. 
Ligi kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012 ilianza kutimua vumbi Agosti 20,2011 na kumalizikia Mei 6, 2012 na kuvishirikisha vilabu 14 vikiwemo  Simba, Yanga, Azam Fc, African Lyon, Kagera Sugar, Mtibwa Sugara, Toto Africans, Moro United, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Coastal Union, Polisi Dodoma na Oljoro JKT.

Comments