VIBOPA WAPYA YANGA WALIPOKUTANA NA WACHEZAJI WAO

 Mwenyekiti mpya wa klabu hiyo Yusuf Manji,akizungumza na wachezaji
 Viongozi wa Kamati ya Utendaji
 Kamati ya Utendaji na viongozi wa klabu
 Wachezaji wakisikila kwa umakini

Manji akisalimiana na Athuman Iddi 'Chuji'

UONGOZI mpya wa klabu ya Yanga leo asubuhi ulitembelea makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na kukutana na kuzungumza na wachezaji. 
Viongozi hao wapya waliokuwepo kwenye msafara huo ni mwenyekiti, Yussuf Manji, makamu mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe wa kamati ya utendaji, Abdalla Bin Kleb, Mussa Katabalo na George Manyama.
Katika msafara huo, pia walikuwemo wajumbe wa kamati ya utendaji katika uongozi uliopita, Salum Rupia na Mohamed Bhinda.
Katika kikao chake hicho na wachezaji, Manji aliwataka wawe na imani kubwa kwa uongozi mpya kwa vile wamejipanga vyema kuhakikisha timu inapata huduma zote muhimu na kwa wakati na pia inapata ushindi katika kila mechi watakazocheza.
Manji aliwaeleza wachezaji hao kuwa, wanapaswa kucheza kwa ari na kujituma kwa vile matatizo yaliyojitokeza msimu uliopita hayatakuwa na nafasi katika uongozi wake.
Katika kikao hicho, wachezaji wa Yanga walionekana kuwa na furaha kubwa huku kila wakati wakipiga makofi ya kumshangilia mfadhili huyo wa zamani wa klabu hiyo.
Mbali na Manji, viongozi wengine waliopata nafasi ya kuzungumza na wachezaji ni Sanga na Katabalo, ambao waliwaelezea mikakati mbalimbali ya uongozi wao.
Manji alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuwabwaga Edgar Chibula na John Jambele. Uchaguzi huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Diamond, Jubilee, Dar es Salaam.
Uchaguzi huo mdogo uliitishwa baada ya kujiuzulu kwa mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga, makamu wake, Davis Mosha na wajumbe wanne wa kamati ya utendaji huku mmoja akifariki dunia.
Picha, habari kwa hisani ya Emmanuel Ndege, mpiga picha wa blogu ya liwazozitoblogspot.com