MAXINSURE YAIPIGA JEKI TWIGA STARS


Ofisa uhusiano wa Maxinsure Amisa Juma akikabidhi sehemu ya msaada waliotoa kwa timu ya Taifa ya Wanawake 'Twiga Stars' kwa ofisa habari wa TFF Boniface Wambura

Kampuni ya bima ya Maxinsure imetoa vifaa vya mazoezi kwa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) vyenye thamani ya sh. milioni 1.3. 
Vifaa hivyo ambavyo ni jezi, bukta na soksi 20, vizibao (bibs) 20 na mipira miwili vimekabidhiwa leo (Julai 12 mwaka huu) kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Amisa Juma. 
Akikabidhi vifaa hivyo, Amisa amesema wamefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya mchango wao kwa jamii lakini vilevile wameamua kuiunga mkono timu hiyo ambayo wanajua haina mdhamini kutokana na vipaji na uwezo ambao umekuwa ukioneshwa na wachezaji wake.
Pia amezitaka kampuni, taasisi, watu binafsi na Serikali kuiunga mkono timu hiyo ili iweze kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali inayotarajia kushiriki.