TOT TAARAB KUWAPA RAHA KANDA YA ZIWA BAADA YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN


Kundi la taarab la Tanzania One Thetre (TOT) chini ya Malkia wa Mipasho nchini, Khadija Omari Kopa litarindima katika mikoa ya Tanga na Kanda ya Ziwa baada ya mfungo huu mtukufu wa Mwezi wa Ramadhani.
Katibu wa TOT, Gasper Tumaini alisema, jana kwamba, ziara hiyo ambayo itatumika kutambulisha albam za ‘Full Stop’ na ‘Mjini Chuo Kikuu’ , itaanza kwa kundi hilo kufanya shoo ya nguvu Tanga katika kurehekea Sikukuu ya Eid El Fitr.
Tumaini alisema, Idd pili, TOT watafunga kazi katika Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga na kumalizia siku ya Iddi tatu katika ukumbi wa White House mjini Muheza mkoani Tanga.
Alisema, baada ya kuwakonga nyoyo wakazi wa Tanga na vitongoji vyake, Khadija Kopa na kundi lake watainua nanga na kwenda kuishusha tena Kanda ya Ziwa, katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Mara na kisha kumalizia Tabora na Singida.
Alisema, mbali na Khadija Kopa, kundi hilo litakuwa na wanamuziki wake wa taarab, wakiwamo Abdul Misambano, Ally Star, Mwamtama Amir ‘Mama Lao’, Mariam Khamis na Mwasiti Suleiman.