TFF YAOMBOLEZA MSIBA WA MELI Z’BAR



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za ajali ya meli ya Mv Skagit iliyotokea jana (Julai 18 mwaka huu) na kupoteza maisha ya karibu abiria 100 waliokuwemo kwenye chombo hicho. 
Ajali hiyo mbaya iliyotokea karibu na Kisiwa cha Chumbe, Zanzibar na kusababisha vifo vya watu wengi ni msiba mkubwa, si kwa wadau wa mpira wa miguu pekee, bali kwa wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
Hivyo tunatoa pole na salamu za rambirambi kwa ndugu wa marehemu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na wote walioathirika na kuguswa na msiba huo mkubwa. 
Kutokana na msiba huo, mechi mbili za leo kuwania Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kati ya Atletico ya Burundi na El Salam Wau ya Sudan Kusini na ile ya Mafunzo ya Zanzibar dhidi ya Tusker ya Kenya zitachezwa huku wachezaji wa timu zote wakivaa vitambaa vyeusi.

Mbali ya vitambaa hivyo, pia kutakuwa na dakika moja ya kukaa kimya kwa ajili ya kuomboleza vifo hivyo kabla ya kuanza mechi hizo zitakazochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mechi ya kwanza itaanza saa 8.00 mchana wakati ya pili itachezwa kuanzia saa 10.00 jioni.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) 

Comments