TFF YAIZODOA KAMATI YA UCHAGUZI YANGA



Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kwa kuzingatia majukumu yake ya kusimamia chaguzi za wanachama wa TFF kama ilivyoanishwa kwenye Katiba ya TFF, Ibara ya 49 (1), na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 26(2) inatoa ufafanuzi ufuatao kuhusu uchaguzi wa kuziba nafasi za uongozi kwenye Klabu ya Yanga:

1.         Wanachama wote wa TFF, ikiwa ni pamoja na Klabu ya Yanga, wanatakiwa kuzingatia kikamilifu Kanuni za Uchaguzi  za Wanachama wa TFF katika kuendesha shughuli zote za uchaguzi.
2.         Wagombea uongozi wote wa wanachama wa TFF wanapaswa kutimiza masharti ya uongozi yaliyoanishwa katika Katiba za vyama vyao na Kanuni za Uchaguzi.
3.         Kamati za Uchaguzi za Wanachama wa TFF zinapaswa kutimiza kikamilifu majukumu yao ya kulinda Katiba za wanachama wa TFF na kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF katika michakato ya uchaguzi. Kamati ya Uchaguzi ya Yanga ilishaelekezwa kufanya hivyo na inakumbushwa kuendelea kuzingatia wajibu huo.
4.         Wagombea uongozi wa wanachama wa TFF wanao wajibu wa kuzifahamu Katiba zao na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF na kuomba uongozi kwa kutimiza matakwa ya Katiba na Kanuni za Uchaguzi.
5.         Kamati ya Uchaguzi ya TFF imepokea maombi ya marejeo (review) dhidi ya uamuzi wake wa kuwaondoa waombaji uongozi wanne (4) wa Klabu ya Yanga. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inatoa uamuzi ufuatao:
i)          Marejeo yaliyoombwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga yanakiuka Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeyakataa. Kamati inafafanua kuwa hata kama Kanuni zingekuwa zinaruhusu kufanya marejeo, bado maombi hayo yasingepaswa kuwasilishwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, bali waombaji uongozi wenyewe. Pamoja na hayo, sababu za kuomba marejeo si za msingi kwa kuwa waombaji uongozi na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga walipewa mwongozo wa kutosha kurekebisha upungufu uliojitokeza katika mchakato wa uchaguzi wa kujaza nafasi za uongozi kwenye Klabu ya Yanga.

ii)         Sara Ramadhani hakutimiza masharti ya kuomba uongozi kwa mujibu wa Ibara ya 10(4) na (5) ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF na kama ilivyoanishwa kwenye Fomu namba 1 kwa kutojaza fomu na kutoambatanisha vithibitisho vya sifa za kugombea. Kwa hiyo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF inasisitiza uamuzi wake na kuitaka Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kuliondoa jina lake katika orodha ya wagombea uenyekikiti wa Klabu ya Yanga.
iii)         Shaaban R. Katwila na Ahmed Waziri Gao wameshindwa kutimiza masharti ya uombaji uongozi kwa kutowasilisha vyeti halisi kwa ajili ya uhakiki kama ilivyotakiwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) baada ya nakala za vyeti vyao kubainika na NECTA kuwa vina utata. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaitaka Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kutekeleza uamuzi wa kuondoa majina yao kwenye orodha ya wagombea uongozi wa Yanga.
iv)        Ramadhan Mzimba Kampira ameshindwa kutimiza masharti ya kugombea uongozi  kama yalivyo kwenye Ibara ya 10(5) ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF kwa kutoambatanisha vithibitisho vya sifa za mgombea. Kwa hiyo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF inasisitiza uamuzi wake na kuitaka Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kuondoa jina lake katika orodha ya wagombea uongozi.
v)         Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaridhia uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Yanga kuwaondoa wafuatao kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi:
(a)        Ally Mayay Tembele
(b)        Abdallah Sharia Ameir
(c)        Jamal Hamisi Kisongo
(d)        Mohamed R Mbaraka

vi)        Wagombea uongozi ambao hawakutajwa hapo juu na ambao walipitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, wametimiza matakwa ya awali ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na hatua za mwisho za uhakiki wa vyeti vya elimu yao, zinaendelea.

Angetile Osiah
KATIBU                       
KAMATI YA UCHAGUZI TFF

Comments