TEMEKE, MWANZA ZAVAANA NUSU FAINALI COPA 2012


Temeke na Mwanza zinapambana kesho (Julai 13 mwaka huu) katika nusu fainali ya kwanza ya michuano ya Copa Coca-Cola 2012 itakayochezwa saa 2.30 asubuhi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. 
Nusu fainali ya pili itaanza saa 9.30 mchana kwenye uwanja huo huo ikizikutanisha timu za Morogoro na Tanga. 
Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na fainali ya michuano hiyo zitachezwa Jumapili (Julai 15 mwaka huu). Mechi ya mshindi wa tatu itaanza saa 5 asubuhi na kufuatiwa na fainali ambayo itafanyika kuanzia saa 9 kamili alasiri.
 Mwanza ilipata tiketi ya nusu fainali kwa kuifunga Kinondoni 3-1 huku Temeke ikitinga hatua hiyo kwa ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Mjini Magharibi. Ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Mara ndiyo ulioipa Morogoro tiketi ya nusu fainali wakati Tanga yenyewe iliilaza Dodoma bao 1-0.